1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vita vya Aleppo vyapamba moto

Mapambano ya kuukamata mji wa Allepo baina ya vikosi vya serikali na waasi yanazidi kupamba moto huko Syria. Waasi sasa wamekiteka kituo muhimu cha ukaguzi kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Uturuki.

Allepo

Aleppo

Kufuatia hali hiyo, Ufaransa imetangaza kutaka kuitisha kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Waasi wamekitwaa kituo hicho cha Anadan kilichopo kaskazini magharibi mwa mji huo wa Aleppo hii leo baada ya mapigano makali yaliyodumu saa10 mfululizo. Hatua hii inawapa uhuru wa kusafiri kwenye maeneo ya kaskazini na Uturuki.

Shirika la Habari la AFP linaarifu kuwa vifaru saba na magari yenye silaha yamechukuliwa na waasi kutoka vikosi vya serikali, huku mengine manane yakiharibiwa vibaya.

FSA: Mapambano yanaendelea

Wanajeshi sita wameuawa kwenye mapigano hayo na wengine 25 wamekamatwa na kuwekwa kizuizini ambapo waasi wanne pia wameuwa. Kamanda wa Jeshi Huru la Waasi wa Syria, FSA, Khalid al Shamsi anasema kuwa mambo ni mazuri kwa upande wao.

Waasi wakiwa kwenye mapambano mjini Aleppo

Waasi wakiwa kwenye mapambano mjini Aleppo

"Hali ni nzuri sana kwetu, tumeuchukua mkoa wa Al Bab na wapiganaji wetu wataendelea kulithibiti jimbo la Aleppo. Sasa tunaimarisha nguvu yetu Aleppo kwa kuwaunganisha wapiganaji wa huko. Tunapata silaha na vifaa kutoka huko na sehemu nyengine za mkoa wa Al Bab". alisema, Kamanda Shamsi.

Mapigano hayo yamewalazimisha kiasi ya raia 200,000 kuukimbia mji huo. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kuna uwezekano mji huo ukakumbwa na janga la kibinaadamu. Mkuu wa umoja huo anayeshughulika na misaada ya kibinaadamu, Valerie Amos, amesema kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu wamekwama kwenye mji huo. Watu wengi wametafuta hifadhi kwenye maeneo ya shule na majengo ya umma. Amos anasema kuwa wanahitaji haraka chakula, magodoro, madawa na maji ya kunywa.

Uamuzi wa Ufaransa

Mataifa ya magharibi yameeendelea na juhudi zao za kukomesha hali hiyo na sasa Ufaransa imetangaza kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta namna ya kusitisha mauwaji hayo.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius

Waziri wa mambo ya Nje wa nchi hiyo, Laurent Fabius, amemuita Rais Bashar al-Assad wa Syria kuwa ni muuwaji na kuutaka umoja huo ufanye kila liwezekanalo kuzuia mauwaji yasiendelee. Fabius amesema kuwa nchi yake itaitisha kikao hicho kabla ya mwisho wa wiki hii.

Ufaransa inatarajia kuchukua kiti cha Urais wa baraza hilo hapo Jumatano. Rais Francois Hollande amesema kuwa atajitahidi kuzishawishi Urusi na China zikubali hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya utawala wa Assad. Nchi za magharibi hadi sasa hazijaweza kukomesha mauwaji ya Syria kutokana na pingamizi za nchi hizo zenye maamuzi ya kura ya turufu kwenye baraza la usalama.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP

Mhariri: Othman Miraji

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com