1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita-Gaza Makombora 10 yashambulia kusini mwa Israel.

Eric Kalume Ponda2 Februari 2009

Kuna hofu ya kuzuka upya kwa mashambulio katika eneo la ukanda wa Gaza kufuatia matukio ya hivi punde ambapo makombora zaidi ya maroketi yamevurumishwa na kushambulia eneo la kusini mwa Israel.

https://p.dw.com/p/GlVa
Waziri wa mambo wa nje wa Israel Tzipi Livni, akitoa onyo kali kwa Hamas.Picha: ap

Choko choko hii imesababisha Israel kutangaza hatua kali kwamba haitasita kuendeleza mashambulio yake ndani ya Gaza baada ya shambulio la hapo jana katika eneo la mji wa mpakani, kujibu mashambulio hayo kutoka upanda wa Gaza.


Ni muda wa wiki mbili sasa tangu Israel kutangaza hatua ya kusimamisha mashambulio na kuwaondoa wanajeshi wake ndani ya Gaza, ili kufuata mkondo wa amani kupitia mpango unaoongozwa na Misri.


Lakini waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert ametoa onyo kali baada ya kikao cha bunge, kwamba huenda ndege za jeshi la nchi hiyo zikapelekwa ndani ya Gaza kufanya mashambzulio, baada ya makombora 10 kuvurumishwa kutoka Gaza na kuwajeruhi watu watatu wakiwemo wanajeshi wawili.


Ndege za jeshi la Israel zilishambulia eneo la mpakani baina ya Gaza na Misri na kuharibu mahandaki na matobwe, yaani njia za chini ya ardhini zinazodaiwa kutumiwa na wafuasi wa Hamas kuingiza silaha ndani ya Gaza.

Mamia ya wakaazi wamelazimika kulihama eneo hilo kwa hofu kwamba huu ni mwanzo mpya wa mashambulio kutoka kwa wanajeshi wa Israel.

Chama cha Hamas, ambacho wajumbe wake wako mjini Cairo kwa mashauriano ya kutafuta amani katika eneo hilo, kimekanusha kuhusika na mashambulio hayo, dai lililopingwa vikali na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel, Tzipi Livni. Livni amesisitiza kuwa Israel haipasi kukubali mpango wa amani na Hamas unaoongozwa na Misri, kwani kufanya hivyo ni kulihalalisha kundi hilo analolitaja kuwa la wapiganaji.


Wajumbe hao wa Hamas wanatarajiwa kufanya mashauriano na mpatanishi mkuu kwenye mpango huo Omar Suleiman ambapo wanatarajiwa kuwasilisha msimamo wa chama hicho kuhusiana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Misri.


Suala hilo liligeuka kuwa la kisiasa nchini Israel pale alipotofautiana vikali na waziri wa ulinzi Ehud Barak ambao wote wanang´ang´ania wadhifa wa waziri mkuu wakati wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 10 mwezi huu.

Ehud Barak amesema kuwa huenda shambulio hilo limetekelezwa na makundi yanayopingana ndani ya Gaza.


Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmmud Abbas ambaye yuko mjini Cairo kufanya mashauriano na mwenzake wa Misri Hosni Mubarak katika juhudi za kufikiwa mkataba wa kudumu wa kusimamisha vita katika eneo hilo, ameyashtumu vikali makundi yanayopingana na chama cha Hamas akisema kuwa yanahatarisha maisha ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza.


Pia kiongozi huyo alishtumu vikali matamshi ya kiongozi wa Hamas anayeishi uhamishoni nchini Lebanon Khaled Meshaal kwamba chama cha ukombozi wa Palestina, PLO, kimepoteza umaarufu wake na kuna haja ya kubadilisha utawala katika maeneo ya Wapalestina.


Chama cha Hamas ambacho si mwanachama wa PLO, kilichukua uongozi wa eneo la Gaza kutoka kwa kundi la Fatah linalomuunga mkono rais Mahmud Abbas mwaka wa 2007.

Wakati huo huo, rais Nicholas Sarkozy ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupitia mataifa ya Umoja wa Ulaya katika juhudi za kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo, anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Qatar Sheikh Abdullah bin Khalifa Al Than kutoa msukumo zaidi kwa mpango huo.


Ponda/Afp-Reuters