1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita- Gaza-Hofu ya mashambulio mapya.

Eric Kalume Ponda27 Januari 2009

Mwanajeshi mmoja wa Israel ameuawa katika eneo la mpakani na Gaza kufuatia shambulio la bomu linalodaiwa kutekelezwa na wafuasi wa Hamas.

https://p.dw.com/p/GhJZ
Mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati George Mitchell akiwasili katika eneo hilo.Picha: AP

Israel pia yadaiwa imejibu kitendo hicho kwa kumuua mwanaharakati wa Kipalestina. Je huu ni mwanzo ukurasa mpya wa mashambulizi katika eneo hilo?


Ndilo swali wanalojiuliza raia wengi wa Ukanda wa Gaza baada ya muda uliotangazwa kusimamisha mapigano hayo kumalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.


Tukio la hivi punde limetajwa kuwa ukiukaji mkubwa wa tangazo la kusimamisha mapigano hayo baina ya pande hizo mbili,lililotolewa kwa januari 18. Maafisa wa huduma za binadamu katika eneo la Gaza, wanasema kuwa hili ndilo shambulio la kwanza kali kutekelezwa tangu hatua ya kusimamisha kwa muda mapigano hayo itolewe.


Hali imeshtumiwa vikali, ikitajwa kuwa inayodudimiza juhudi za jamii ya kimataifa kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo la mashariki ya kati. Shambulio hilo limetokea huku mjumbe maalum wa Rais Barack Obama katika eneo hilo la mashariki ya kati George Mitchell, akielekea eneo hilo kufanya mazungumzo na viongozi wa kanda hiyo, katika juhudi za kutoa msukumo zaidi kwa mpango wa amani.

Rais Barack Obama amsema kuwa, amani ya kudumu katika eneo hilo, kamwe haiwezi kupatikana kwa mtutu wa bunduki


Rais Obama alisema ``Nina amini kuwa huu ni wakati muafaka kwa pande hizo mbili kutambua kwamba njia wanayoifuata haiwezi kuutatua mzozo huu na kuleta amani ya kudumu kwa raia wa eneo hilo. Na badala yake wanapaswa kurejea katika meza ya mazungumzo. Naelewa kuwa haitakuwa kazi rahisi na itachukua muda mrefu, lakini kwa ushirikiano na mataifa mengine kama vile Russia, umoja wa Ulaya na mataifa ya Kiarabu bila shaka tutalipatia ufumbuzi´´.


Baada ya ziara hiyo, George Mitchel anatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yake kwa utawala wa Rais Barack Obama, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya binadamu kwa raia wa Gaza kufuatia mashambulio yaliyodumu kwa muda wa siku 22.

Huku hayo yakijiri waziri wa maongozi ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana amefanya mashauriano na Rais Hosni Mubarak wa Misri mjini Cairo kuhusiana na suala hilo la Gaza.


Viongozi hao wawili walijadilia suala la kufunguliwa kwa maeneo ya mpakani ili kutoa nafasi ya kuingizwa kwa misaada ya binadamu na kadhalika kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo.


Umoja wa Ulaya ambao umekuwa katika mstari wa mbele kutafuta amani ya eneo hilo la Mashariki ya kati,siku ya Jumatatu wiki hii ulitangaza kiasi cha Euro milioni 58 kusaidia juhudi a misaada ya binadamu katika eneo la Gaza lililoharibiwa wakati wa vita hivyo.


Pia walizungumzia juhudi za kuyapatanisha makundi mawili hasimu katika eneo la Gaza ikiwa ni kundi la Fatah na Hamas.


Makundi hayo mawili yanatarajiwa kurejea katika meza ya mazungumzi mjini Cairo Misri February 22. Hata hivyo kiongozi wa chama cha Hamas Salah el-Bardawi amenukuliwa akisema kuwa huenda mahsauriano hayo yasifanyike iwapo wanachama wao anayezuiliwa na kundi la Fatah katika eneo la ukingo wa magharibi hataachiliwa huru.


Uhusiano wa makundi hayo mawili ulizorota baada ya chama cha Hamas kuchukua uongozi wa eneo la Gaza kutoka kwa Rais Mahmud Abbas mnamo Juni 2007.


Ponda/Afp