1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wanawasi wasi na uchumi wa dunia.

27 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CyDV

Davos.

Kikao cha Jumamosi cha medani ya kiuchumi ya dunia mjini Davos, Uwisi, kimegubikwa katika hali ya wasi wasi. Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF, Dominique Strauss-Kahn, amesema matatizo yanayokabili uchumi wa dunia ni makubwa na yanahitaji jibu mjarabu ikiwa ni pamoja na upunguzaji wa viwango vya riba na kuongeza matumizi ya serikali.

Hofu ya kuporomoka kwa uchumi wa Marekani na uchumi wa dunia , masoko ya hisa yanayoyumba yumba pamoja na kashfa ya benki ya Ufaransa ya Sociate Generale yanazidisha hali mbaya ya utabiri jumla wa hali ya uchumi mjini Davos. Waziri wa fedha wa Ufaransa Christine Lagarde amesema kuwa mkutano wa Davos ni muhimu kwa masuala ya kilimwengu.

Wakati huo huo , mkuu wa shirika la biashara la dunia WTO , Pascal Lammy, amesema kuwa uamuzi wa kuitisha mkutano wa mawaziri ili kufufua mazungumzo ya kibiashara ya Doha utafanyika katika muda wa wiki chache zijazo.

Mawaziri wanaohudhuria mkutano huo wa kiuchumi wa dunia wameonyesha kuwa mataifa masikini na tajiri yanaweza kukutana wakati wa sherehe za pasaka kujaribu kupata makubaliano ambayo yamekuwa hayapatikani kwa muda mrefu duniani. Makubaliano ya kibiashara kama hiyo yanaweza kuongeza hali inayohitajika ya kujiamini katika uchumi wa dunia wenye matatizo, na kusaidia kuondosha hali ya kuhami masoko.