1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wahotubia Baraza Kuu

P.Martin25 Septemba 2007

Rais George W.Bush wa Marekani,amelihotubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,akizungumzia haki za binadamu hadi suala la kufuta umasikini.Kwa upande mwengine,Rais wa Iran,Mahmoud Ahmedinejad, ambaye nchi yake ni hasimu mkubwa wa Marekani,anatarajiwa pia kulihutubia baraza hilo kuu baadae hii leo.

https://p.dw.com/p/CB10

Rais Bush amesema,Marekani ina jukumu mahsusi la kuchukua uamuzi wa kupunguza vikwazo vya kibiashara.Akasisitiza kwamba nchi yake itapigania kupatikane mafanikio katika mazungumzo ya kibiashara yanayojulikana kama Duru ya Doha.

Kuhusu suala la haki za binadamu,rais huyo wa Marekani alielezea kutoridhishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kutoa wito wa kufanywa marekebisho katika baraza hilo. Aidha alisema,Marekani itaweka milango wazi kuhusu mazungumzo ya mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Lakini pamoja na hayo,aliitaja kwa jina Japani akisema,ni nchi inayostahiki kuwa mwanachama wa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bush vile vile alitoa wito wa kuongezwa mbinyo dhidi ya serikali ya Zimbabwe,wakati mamilioni wakilazimika kuihama nchi yao kuukimbia utawala wa Mugabe.Amesema,jumuiya ya kimataifa haina budi kupigania mabadiliko nchini Zimbabwe kwa ajili ya uhuru wa umma wa nchi hiyo.

Kadhalika alizungumzia hali ya mambo nchini Myanmar ambayo hapo zamani ilikuwa ikijulikana kama Burma.Amesema,Marekani itasimama upande wa wanaopigania demokrasia na haki;na dhidi ya utawala wa kijeshi katika taifa hilo la Asia.

Alimpongeza pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon kwa juhudi zake kuhusiana na suala la hifadhi ya mazingira.

Katibu Mkuu huyo jana aliufungua mkutano wa kilele wa siku moja kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na aliwahimiza viongozi wa nchi mbali mbali kujitahidi kupata maafikiano,watakapokutana Bali nchini Indonesia mwishoni mwa mwaka.Lengo la mkutano huo utakaofanywa kuanzia tarehe 3 hadi 14 mwezi wa Desemba,ni kupata mkataba mpya wa kimataifa,kuhusu njia za kutenzua tatizo la ongezeko la ujoto duniani.Hata Rais Bush katika hotuba yake leo hii,alieleza juu ya azma ya Marekani,kutoa ushirikiano wake ili kufikia lengo hilo.

Baada ya Bush,ilifuata hotuba ya Rais wa Ghana, John Kofour ambae nchi yake hivi sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Baadae jioni hii Rais wa Iran,Mahmoud Ahmedinejad ambaye nchi yake ni hasimu mkubwa wa Marekani anatarajiwa kulihutubia baraza hilo kuu.Iran imo katika mvutano na nchi za magharibi,kuhusiana na mpango wake wa nyuklia,huku serikali ya Tehran ikishilia kwamba mradi huo ni kwa ajili ya matumizi ya amani tu.Lakini nchi za magharibi zina wasi wasi kuwa Iran huenda ikawa ina ajenda ya siri ya kutaka kuunda silaha ya nuklea.