1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana baadae hii leo mjini Brussels

23 Juni 2011

Ajenda kuu ya mkutano wao wa kilele ni kuhakikisha uwezo wao wa kuumaliza mgogoro usiokwisha wa deni la Ugiriki, na kuepusha balaa la mgogoro huo kuenea katika zoni ya Euro.

https://p.dw.com/p/11i8E
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao december mwaka jana mjini BrusselsPicha: AP

Hakuna maajabu yoyote yanayotazamiwa kutokea wala uamuzi mpya utakaopitishwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili utakaoanza leo usiku mjini Brussels. Labda mawaziri wa fedha watakapokutana kama ilivyopangwa July tatu ijayo.

Katika wakati ambapo umoja wa sarafu ya Ulaya unazongwa na migogoro, viongozi wa taifa na serikali wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wanapanga kuthibitisha utayarifu wao wa kuipatia Ugiriki msaada ziada katika awamu ya kwanza ya mpango wa kuiokoa nchi hiyo ulioanzishwa mwaka mmoja uliopita, kwa sharti kama wiki ijayo bunge la Ugiriki litaidhinisha mpango wa kufunga mkaja uliokubaliwa baada ya majadiliano pamoja na wafadhili wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa nchi za Ulaya, viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya watabidi "watoe dhamana inayotakiwa na shirika la fedha la kimataifa" ili Ugiriki iweze kupatiwa fedha taslimu ifikapo mwezi ujao wa July.

Demonstrationen vor dem griechischen Parlament
Wagiriki waandamana kupinga hatua za kufunga mikajaPicha: dapd

Kitisho cha kufilisika Ugiriki hakiwashughulishi peke yao viongozi wa Umoja wa Ulaya. Ni kitisho kinachoushughulisha ulimwengu mzima-amesema hayo John Lipsky, ambae ni mwenyekiti wa muda wa shirika la fedha la kimataifa, IMF na kuendelea

"Mnauliza kama mambo yatakwenda kombo. Sisi tunajitahidi kuona na kuhakikisha mambo yanapita vizuri."

Mbali na mgogoro wa Ugiriki, mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unatazamiwa kuidhinisha hatua kadhaa zilizolengwa kuhifadhi sarafu ya Euro dhidi ya migogoro.

NATO-Angriff auf Libyen
Madege ya NATO yapiga katika eneo wanakoishi raia mjini TripoliPicha: picture-alliance/dpa

Kesho itakuwa zamu ya kuzungumzia suala la Libya katika wakati ambapo lawama zinazidi kusikika dhidi ya kuendelea opereshini za jumuia ya kujihami ya NATO nchini humo na pia mzozo wa Syria.

Viongozi wa taifa na serikali watazungumzia pia kuhusu wahamiaji. Suala la kufanyiwa marekebisho mkataba wa Schengen litazingatiwa, na hivyo kurahisisha uwezekano wa kuendelezwa ukaguzi wa mpakani, ikilazimika.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,Reuters

Mhariri:Miraji Othman