1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kuhutubia kongamano la kiuchumi Davos

Grace Kabogo
24 Januari 2018

Kongamano la Kiuchumi Duniani, WEF leo linaingia katika siku yake ya pili mjini Davos, Uswisi ambapo viongozi wa mataifa makubwa barani Ulaya wanatarajia kuzungumzia mtazamo wao kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2rQ8v
Frankreich Merkel bei Macron
Picha: picture alliance/dpa/POOL EPA/C. P. Tesson

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel anatarajiwa kuzungumza mchana wa leo kuhusu mipango ya mageuzi makubwa katika Umoja wa Ulaya, iliyopendekezwa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Macron atazungumza kwa mara ya kwanza katika kongamano hilo la kiuchumi tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Ufaransa, ambapo pia atagusia kuhusu hali ya sasa ya utandawazi.

Kwa mujibu wa duru za karibu za ofisi ya Macron, kiongozi huyo atazungumzia changamoto tatu zinazoikabilia dunia ambazo ni kutofautiana kwa usawa katika uchumi na masuala ya kijamii, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uongozi wa dunia katika nyanja ya uzalend o na itikadi kali.

Präsident Donald Trump
Rais Donald TrumpPicha: picture alliance/abaca/O. Douliery

Kwa upande wake Kansela Merkel ataelezea jinsi bara la Ulaya lilivyogeuka baada ya miaka mingi ya mzozo wa kiuchumi. Viongozi hao watazungumza siku mbili kabla ya Rais wa Marekani, Donald Trump hajahutubia katika kongamano hilo. Mfalme wa Uhispania, Filipe wa Sita pia atazungumza na washiriki wa kongamano hilo na chochote atakachokizungumzia kuhusu jimbo la Catalonia, kinaweza kuwa na maslahi. Viongozi wengine watakaozungumza leo ni Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni na Rais wa Brazil, Michel Temer.

Viongozi hao watazungumza baada ya jana India na Canada kupinga msimamo wa Trump wa kujilinda. Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alitoa hotuba ya ufunguzi katika kongamano hilo kwa kutetea biashara huria. Baadae Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau aliusifu mkataba wa biashara kati ya nchi 11 za Asia na Pasifiki, kwa lengo la kuziba ule ambao Trump alijiondoa mwaka uliopita.

Merkel kukutana na wafanyabiashara wa Afrika

Merkel pia anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pamoja na Rais wa Argentina, Mauricio Macri. Macri amerithi kiti cha Merkel kama rais wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea na yanayoinukia kiuchumi, G20. Merkel pia anapanga kupata chakula cha mchana pamoja na wafanyabiashara wa Afrika na Ujerumani, kama sehemu ya juhudi za Ujerumani kuimarisha maendeleo na kukabiliana na uhamiaji.

Schweiz Davos - Indiens Premierminister Narendra Modi beim World Economics Forum (WEF)
Waziri Mkuu wa India, Narendra ModiPicha: Reuters/D. Balibouse

Hata hivyo, kabla ya hotuba itakayotolewa na Trump siku ya Ijumaa, Waziri wa Uchumi wa Marekani, Steven Mnuchin amesema kuwa nchi yake inajizatiti kabisa katika biashara huru na ya haki. Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na waandishi habari katika Kongamano la Kiuchumi Duniani mjini Davos, siku mbili baada ya Trump kusaini vipengele vipya vya ushuru wa kuingiza vifaa vinavyotumia nishati ya jua pamoja na mashine kubwa za kufulia nguo.

Wakati huo huo, maelfu ya watu wameandamana mjini Zurich kupinga kuwasili kwa Trump ili kuhudhuria kongamano hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman