1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa SADC wakutana na Rais Mugabe.

7 Mei 2008

Wakati Ulimwengu ukisubiri kufanyika kwa duru ya pili ya Uchaguzi nchini Zimbabwe, nchi hiyo tayari inakabiliwa na machafuko mapya juu ya suala hilo la uchaguzi.

https://p.dw.com/p/DvlO
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.Picha: AP

Hali hii inakuja baada ya chama tawala na chama cha Upinzani kuwasilisha changamoto za kisheria dhidi ya nusu ya matokeo ya Uchaguzi wa Bunge uliofanyika mwezi Machi.

Wakati huo huo Viongozi wa SADC wamekutana na Rais Mugabe leo.

Gazeti moja la Serikali la Herald, limesema kwamba Chama Tawala cha ZANU-PF, kinacho ongozwa na Rais Robert Mugabe, ambacho kwa mara ya kwanza kilipoteza wingi wa wawakilishi katika bunge kwenye Uchaguzi uliofanyika mwezi Machi, sasa kilikuwa kinashindania majimbo hamsini na tatu kati ya majimbo mia mbili na kumi wakati upande wa Upinzani ulikuwa unashindania tena majimbo hamsini na mbili.

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika umezitaka pande zote mbili kusitisha vurugu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mwingine wakati upinzani unadai kuwa tayari wafuasi wake ishirini na tano wameshauawa tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Kutokana na wingi wa kesi zilizowasilishwa katika mahakama ya Uchaguzi, zimemfanya jaji Mkuu wa Mahakama hiyo kuteua majaji wengine kumi na saba ili waweze kusaidia.

Jaji wa Mahakama Kuu, Charles Nyatanga, amenukuliwa akisema kuwa tayari wameshapokea kesi mia moja na tano ambazo zinapaswa kushughulikiwa katika kipindi cha miezi sita tu kwa kufuata sheria ya Uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi iliona kuwa chama tawala cha ZANU -PF,kikipoteza uwakilishi mwingi katika Bunge, hii ikiwa ni mara ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake miaka ishirini na nane iliyopita.

Kwa upande mwingine, Mawaziri wawili ambao pia ni Wawakilishi wa Ngazi za juu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika,-SADC, wamekutana leo na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kwa lengo la kujadili hali ya kisiasa nchini humo na kushawishi kuendelea kwa duru ya pili ya Uchaguzi.

Wawakilishi hao wa SADC, wamekutana na Rais Mugabe Mjini Harare ambako wamemtaka kuendelea na duru hiyo ya pili ya uchaguzi lakini kwa kuzingatia sheria.

Uwakilishi huo uliongozwa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Angola Jose Joao Bernardo Miranda, ambaye ni msimamizi wa baraza la SADC, linaloshughulikia masuala ya Usalama na Siasa.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown, amezitaka nchi jirani za Afrika kutia nguvu ili kuhakikisha kuwa duru ya pili ya Uchaguzi nchini Zimbabwe inafanyika kwa uhuru na haki.

Bwana Brown amerejea tena wito wake wa kuruhusiwa kupelekwa kwa waangalizi zaidi nchini Zimbabwe kwa ajili ya kuangalia jinsi uchaguzi utakavyoendeshwa ili kuondoa mtazamo wa kuwa huwenda rais Mugabe anataka kubatilisha pia duru ya pili ya uchaguzi.

Amesema Uchaguzi huo unapaswa kusimamiwa na waangalizi kutoka Jumuia zote za Kimataifa ili kuhakikisha unakuwa wa Huru na Haki ili kulinda haki na usalama kwa raia wa Zimbabwe.

Uingereza ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa Zimbabwe, mapema wiki hii ilitoa wito wa kupelekwa kwa waangalizi wa Kimataifa nchini humo haraka iwezekanavyo ili uchaguzi huo upate fulsa ya kuwa wa halali.

Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani cha MDC, Morgan Tsvangirai amekuwa akitishia kususia kushiriki duru ya pili ya uchaguzi akiamini kuwa alishinda kwa zaidi ya asilimia hamsini katika awamu ya kwanza ya Uchaguzi na hivyo haoni sababu yoyote ya kurudiwa kwa uchaguzi huo.