1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya tabia nchi mkutanoni

8 Juni 2015

Viongozi wa G7 wamekubaliana katika mkutano wao wa kilele katika kasri la Elmau kuhusu kupunguzwa kwa sehemu kubwa moshi wa sumu unaotoka viwandani na kuimarishwa vikwazo dhidi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/1FdcN
Viongozi wa mataifa Saba tajiri zaidi kiviwanda katika mkutano wao katika kasri la ElmauPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Suala la mabadiliko ya tabia nchi liligubika mazungumzo mnamo siku hii ya leo,ya pili na ya mwisho ya mkutano wa viongozi wa mataifa saba tajiri zaidi kiviwanda G7 katika kasri la Elmau katika jimbo la kusini la Bavaria.Kansela Angela Merkel amepania kuona makubaliano yanafikiwa kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utakaofanyika mwezi decemba mwaka huu mjini Paris nchini Ufaransa.

Katika taarifa yao ya mwisho viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda G7 wamezungumzia umuhimu wa kuwekwa lengo maalum la kupunguza kati ya asili mia 40 hadi 70 hadi ifikapo mwaka 2050 kiwango cha moshi wa sumu unaotoka viwandani ikilinganishwa na hali namna ilivyokuwa mnamo mwaka 2010.

Pande zinazohasimiana zatakiwa ziheshimu makubaliano ya Minsk

Kuhusu mzozo wa Ukraine viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda wameionya Urusi itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi kutokana na "uchokozi wake" nchini Ukraine."Tuko tayari kupitisha hatua kali zaidi dhidi ya Urusi ikilazimika"viongozi hao wamesema katika taarifa yao ya pamoja.Viongozi wa Urusi wametakiwa waheshimu makubaliano ya Minsk pamoja na kutambua milki ya Ukraine.Hapo awali kansela Angela Merkel alizitolea wito pande zote mbili,Urusi na Ukraine ziheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha yaliyofikiwa february 12 katika mji mkuu wa Byelorusi-Minsk.

G7 Gipfel Merkel Abschluss PK
Kansela Angela Merkel akihitimisha mkutano wa kilele wa G7Picha: Reuters/M. Rehle

Kuhusu mgogoro wa madeni wa Ugiriki mataifa tajiri kiviwanda G7 yamesema yanapendelea kuiona Ugiriki ikiendelea kuwa mwanachama wa kanda ya Euro.Hata hivyo wanasema mshikamano pamoja na Ugiriki unamaanisha Athens itekeleze ahadi ilizotoa za mageuzi.

ISIL watashindwa tu asema Obama

Kitisho cha mashambulio ya wafuasi wa itikadi kali wa IS na mapambano dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram nayo pia yalijadiliwa.

G7 Gipfel Schloss Elmau Outreach Konferenz Merkel und Nkosazana Dlamini-Zuma
Kansela Merkel akiamkiana na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika bibi Nkosazana Dlamini-Zuma ambae ni miongoni mwa viongozi wac Afrika walioalikwa kuhudhuria mkutano wa G7Picha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Akizungumza na waziri mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi,rais wa Marekani Barack Obama amesema ana matumaini mema wanamgambo wa itikadi kali wa dola ya kiislam watatimuliwa kutoka Iraq.Abadi ameihimiza jumuia ya kimataifa iwasaidie kuwazuwia wanamgambo wa daesh wasijitajirishe kwa biashara ya chini kwa chini ya mafuta ya nchi hiyo.

Kuhusu Libya viongozi wa G7 wamezitolea wito pande zote zinazohasimiana zipitishe maamuzi ya kijasiri katika mkutano unaosimamiwa na umoja wa mataifa nchini Moroko."Wakati wa mapigano umepita,umewadia wakati wa kusaka ufumbuzi wa kisiasa"amesema viongozi wa G7 katika taarifa yao ya mwisho huko Elmau.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP/AFP/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu