1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa maandamano Sudan waliokamatwa waachiwa

John Juma
10 Juni 2019

Viongozi wenye ushawishi wa vuguvugu la maandamano Sudan waliokamatwa wiki iliyopita wameachiwa huru. Wakati huo huo wanajeshi zaidi wamepelekwa sehemu mbalimbali Sudan kuimarisha usalama.

https://p.dw.com/p/3K8cO
Wanajeshi maalum wa kukabiliana na hali ya dharura pamoja na wa kawaida wamepelekwa sehemu mbalimbali Sudan ili kurejesha hali ya kawaida.
Wanajeshi maalum wa kukabiliana na hali ya dharura pamoja na wa kawaida wamepelekwa sehemu mbalimbali Sudan ili kurejesha hali ya kawaida.Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Babiker

Maafisa nchini Sudan wamewaachilia huru viongozi watatu wa waasi wenye ushawishi mkubwa ambao walikamatwa na kuwekwa kizuizini wiki iliyopita. Hayo yanajiri wakati uasi wa kiraia ulioitishwa na wakuu wa waandamanaji dhidi ya baraza la mpito la jeshi ukiendelea kwa siku ya pili. Jeshi limewalaumu wakuu wa waandamanaji kwa kuendeleza vurugu na limewatuma wanajeshi zaidi kushinka doria.

Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya Sudan kimeripoti leo kuwa viongozi hao watatu wenye ushawishi, Yasir Arman ambaye ni naibu mkuu wa vuguvugu la Sudan people's Liberation Movement-North (SPLM-N), pamoja na waasi wengine wawili wakuu wa vuguvugu hilo Ismail Jalab na Mubarak Ardol waasi wawili wamechiwa huru, lakini hakikufafanua waliachiwa huru lini.

Arman aliwasili mjini Khartoum mnamo Mei 26, kushiriki kwenye mazungumzo na majenerali wa kijeshi waliochukua uongozi baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa rais wa muda mrefu Omar Al-Bashir mwezi Aprili. Hatua iliyojiri kufuatia maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya uliokuwa utawala wake wa kimabavu.

Arman alikamatwa Juni 5, siku mbili baada ya watu waliovalia magwanda ya kijeshi kuvunja maandamano ya wiki kadhaa nje ya makao makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100, wameachiliwa huru.

Jalab na Ardol walizuiliwa katika makaazi yao baada ya kukutana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliyezuru Sudan wiki iliyopita kujaribu kuwapatanisha majenerali na wakuu wa waandamanaji ili kufufua mazungumzo kati yao.

Waandamanaji wameitisha uasi wa kiraia dhidi ya baraza la mpito la kijeshi Sudan
Waandamanaji wameitisha uasi wa kiraia dhidi ya baraza la mpito la kijeshi SudanPicha: Reuters

Tangu mwaka 2011, tawi la SPLM_N lenye silaha limekuwa likipambana na vikosi vya serikali ya rais wa zamani Bashir, eneo la Blue Nile na majimbo ya kusini mwa Kordofan.

Kundi hilo la waasi ni sehemu ya vuguvugu linalopigania uhuru na kuandaa maandamano yaliyouangusha utawala wa Bashir.

Kuachiwa kwa Arman ilikuwa mojawapo ya masharti yaliyowekwa na vuguvugu la waandamanaji kabla ya kuanza upya mazungumzo yoyote na majenerali.

Tangu kupinduliwa kwa Bashir, maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakikita kambi nje ya makao makuu ya jeshi wakitaka baraza la mpito la jeshi kuachia utawala wa kiraia madaraka.

Baraza la kijeshi la mpito limelishutumu vuguvugu linaloongoza maandamano nchini humo kwa kuendeleza machafuko.

Hapo jana watu wanne waliuawa wakati maafisa wa usalama walikuwa wakitawanya maandamano kutokana na uasi wa kiraia ulioanzishwa na waandamanaji walioweka vizuizi na kuziba barabara.

Baraza hilo la jeshi limesema kwa kuziba barabara na kuweka vizuizi, waandamanaji walifanya uhalifu.

Baraza hilo limewapeleka wanajeshi katika maeneo mbalimbali ili kurejesha hali ya kawaida.