Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini kufanya mkutano wa kihistoria | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 08.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini kufanya mkutano wa kihistoria

Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini wanakutana mwezi huu kuimarisha uhusiano kati yao.Hii itakuwa mara ya pili kwa mataifa hayo mawili kufanya mkutano katika kipindi cha miaka saba iliyopita.Kikao hicho kinalenga kuimarisha ushirikiano wa miradi ya uchumi hasa baada ya viwanda vya nuklia vya Pyongyang kufungwa .

Mpaka wa Korea Kusini na Kaskazini ulio na ulinzi mkali kote ulimwenguni

Mpaka wa Korea Kusini na Kaskazini ulio na ulinzi mkali kote ulimwenguni

Mkutano huo kati ya viongozi hao wawili unaandaliwa na Rais Wa Korea Kaskazini Kim Jong Il na kupangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu mjini Pyongyang.

Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini wanakutana mwezi huu ikiwa ni mara ya pili tangu rasi ya Korea kugawanywa baada ya vita vya pili vya dunia.Hatua hii inafanyika baada ya Korea Kaskazini kufungwa viwanda vyake vitano vya nuklia shughuli iliyosimamiwa na waangalizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia matumizi ya nuklia IAEA.

Mkutano wa kwanza kati ya mataifa hayo mawili ulifanyika mwezi Juni mwaka 2000 pale Rais Kim Jong Il alipokutana na Rais wa Korea Kusini wa kwa wakati huo Kim Dae-Jung.Kikao hicho aidha kilifanyika katika mji mkuu wa Korea Kaskazini wa Pyongyang.Mataifa hayo mawili ya Korea yanazozana kimsingi tangu vita kati vya Korea kumalizwa kwa makubaliano ya kusitisha vita wala sio makubaliano ya amani.

Hata hivyo mkutano wa mwaka 2000 ulisababisha ushirikiano wa miradi ya kibiashara aidha kuwaleta pamoja jamaa wanaotengwa kwasababu ya mpaka wao wa pamoja.Mpaka huo ndio ulio na ulinzi mkali zaidi ulimwenguni.

Rais wa Korea Kusini Roh Moo-yung aliwaeleza maafisa wa usalama kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha uhusiano kati yao na Kaskazini ambao umeharibika kwasababu ya mpango wa nuklia wa nchi hiyo.Kiongozi huyo anaongeza pia kuwa mkutano huo utasaidia kuimarisha uhusiano wa Korea Kaskazini na jamii ya kimataifa.

Kiongozi wa zamani wa Korea Kusini Kim Dae-Jung aliyeandaa mkutano wa kwanza miaka 7 iliyopita anapokea vizuri habari za kikao hicho.Kwa mujibu wa taarifa yake mkutano huo ni hatua kubwa ya kutafuta amani kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande mwingine chama cha upinzani cha Grand National Party GNP kinapinga hatua hiyo kwa madai kuwa madhumuni ya kikao hicho ni kumpigia debe mgombea anayependwa na Rais Roh Moo-hyun wakati uchaguzi unasubiriwa kufanyika mwezi Disemba. Kulingana na chama hicho mkutano huo hauna ajenda inayokubaliwa na umma na huenda ikapelekea hatua ya kuipa msaada mkubwa Korea Kaskazini ili kuwavutia.Kwa mujibu wa kura ya maoni wagombea wa chama cha upinzani cha GNP wanaongoza na kuwa na ushawishi mkubwa.

Mtizamo huo unaungwa mkono na kiongozi wa kundi la kisheria la Newright Union Civic bwana Jhe Seong-Ho anayeongeza kuwa kikao hicho kinalenga kuwapigia debe wagombea wanaounga mkono serikali.Baadhi ya wanaharakati walioandamana karibu na afisi ya rais waliteketeza bendera ya Korea Kaskazini aidha kunyunyiza wino ili kufuta picha za viongozi hao wawili watakaokutana.

Vyama vinavyounga mkono serikali mfano Chama cha Uri kilichoanzishwa na Rais Roh kinatumai kuwa mkutano huo utatafuta ufumbuzi kwa masuala tete likiwemo kusitishwa kwa mpango wa nuklia wa Korea Kaskazini.Mashirika ya kibiashara nayo yanunga mkono mkutano huo yakitumai kuwa ushirikiano wa kibiashara utaimarika.

Jamii ya Kimataifa inapokea vizuri tangazo la mkutano huo na kuongeza kuwa utaimarisha juhudi za kimataifa za kusalimisha Korea kaskazini.Marekani inatumai kuwa mazungumzo hayo yatatimiza malengo ya mazungumzo ya pande sita yanayoazimia kusitisha mpango wa nuklia wa Korea kaskazini na badala yake kupata msaada wa nishati na uhusiano wa kidiplomasia.

Mazungumzo ya pande sita yanaleta pamoja mataifa ya Korea Kusini na Kaskazini,Uchina,Japan,Marekani na Urusi.Japan kwa upande wake inakataa kufadhili mpango wa msaada kwa Korea kaskazini ndipo isitishe mpango wake wa nuklia.Kulingana na Japan Korea Kaskazini sharti isuluhishe mzozo kati yao kufuatia kutekwa kwa raia wake katika miaka ya 70 na 80.

Hata hivyo inaunga mkono mkutano huo wa mwishoni mwa mwezi huu.

Uchina iliyo mwandani wa pekee wa kimataifa wa Korea Kaskazini inatarajia matokeo mazuri ya mazungumzo hayo.

 • Tarehe 08.08.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB26
 • Tarehe 08.08.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB26

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com