1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiarabu na Kiafrika wakutana Kuwait

Oumilkher Hamidou19 Novemba 2013

Viongozi wa mataifa ya kiarabu na kiafrika wanakutana mjini Kuwait kutafakari uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Ghuba, tajiri kwa mafuta na bara la Afrika linalohitaji wawekezaji.

https://p.dw.com/p/1AKff
Wenyeji wa mkutano wa viongozi wa kiarabu na kiafrika:Mfalme wa Kuwait Sheikh Sabah al Ahmed al-Sabah (kulia) na mwanamfalme Sheikh Nawaf al Ahmed al-SabahPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano huo wa kilele wa siku mbili ni wa kwanza wa aina yake tangu mwaka 2010, tarehe ambayo viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya nchi za kiarabu na Umoja wa Afrika walikutana nchini Libya muda mfupi kabla ya wimbi la mageuzi la msimu wa kiangazi kupiga na kuzing'owa tawala zote za kiimla ikiwa ni pamoja na ule wa mjini Tripoli.

Viongozi 30 wa taifa, makamo saba wa rais na mawaziri wakuu watatu wamethibitisha watahudhuria mkutano huo wa kilele unaotarajiwa kuwakaribisha pia wajumbe kutoka zaidi ya nchi na mashirika 71.

Washiriki wanatarajiwa kuidhinisha nyaraka na maazimio kadhaa yaliyopitishwa Jumapili iliyopita na mawaziri wao wa mambo ya nchi za nje, yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili zinazojumuisha mataifa tajiri ya kifalme ya Ghuba la Uajemi na pia mataifa ya kiafrika yanayotajwa kuwa miongoni mwa mataifa maskini kabisa ya dunia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kuwait, Sheikh Sabah Khaled al Sabah, amesema mkutano huu wa kilele ambao kauli mbiu ni "Ushirikiano kwa ajili ya Maendeleo na Uwekezaji" utazungumzia njia za kubuni soko la pamoja na nchi za kiafrika na kiarabu kwa ajili ya wakaazi wao bilioni 1.2.

Washiriki mkutanoni watajadili pia kuhusu namna ya kuharakisha raslimali kuelekea Afrika, bara lenye utajiri mkubwa wa mali ghafi lakini linalosumbuliwa na ukosefu mkubwa wa vitega uchumi.

Kwa mujibu wa benki kuu ya dunia, bara la Afrika linahitaji takriban dola bilioni 30 kuwekezwa katika sekta za nishati na umeme.

Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, linasema ukuaji wa kiuchumi barani Afrika umefikia asilimia 5 mwaka jana. Kiwango hicho kinaweza kupungua kidogo mwaka huu na kusalia asilimia 4.8, kabla ya kupanda upya hadi asilimia 5.1 mwakani.

Zaidi ya hayo Afrika inamiliki asilimia 12 ya akiba jumla ya mafuta ulimwenguni na asilimia 42 ya madini ya dhahabu. Kugunduliwa hivi karibuni gesi katika maeneo ya mwambao wa mashariki ya Afrika ni ongezeko pia kwa neema ya kiuchumi ya bara hilo.

Mkutano wa kilele ulioitishwa Libya miaka mitatu iliyopita ulipitisha mkakati wa ushirikiano kati ya nchi za kiarabu na kiafrika pamoja na mpango wa kimkakati kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2016, lengo likiwa kuongeza vitega uchumi, biashara na miradi ya pamoja ya kiuchumi.

Lakini utekelezaji wake ulidorora kwa sehemu kutokana na machafuko ya tangu mwaka 2011 katika nchi zilizokumbwa na vuguvugu la mageuzi ya msimu wa kiangazi nchini Tunisia, Libya, Misri na Yemen na pia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mkutano wa kilele utadurusu mpango wa kuanzishwa mkakati wa kifedha utakaorahisisha kupatikana njia zinazohitajika katika kutekeleza miradi ya pamoja na kuhimiza shughuli za uwekezaji kati ya pande hizo mbili.

Kamati ya ushirikiano ya nchi za kiafrika na kiarabu itaundwa pia kuwashughulikia wahamiaji na kuwalinda wafanyakazi wa kigeni pia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Josephat Charo