1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Isreal na Palestina wajaribu kuyafufua mazungumzo ya amani yaliyokwama

Siraj Kalyango27 Desemba 2007

Mahmud Abbas wa Palestina ailaumu Israel kwa kukwamisha mazungumzo

https://p.dw.com/p/Ch1Q
Mwanajeshi wa Israel akiwa juu ya deraya katika ulinzi wa mwanya katika ukuta unaojengwa ukitenganisha eneo la West Bank na Israeli wa Qalqiliya kutoka Kfar Saba nchini Israel.Picha: AP

Viongozi wa Israel na Palestina wanajaribu kufufua mazungumzo ya amani ambayo yalikwama baada ya vikao viwili tu kutokana na suala la makazi ya waIsrael.

Waziri Mkuu wa Israel-Ehud Olmert amekuwa mwenyeji wa kiongozi wa Palestina-Mahmud Abbas nyumbani kwake mjini Jerusalem kwa mkutano wao wa kwanza tangu wafufue mazungumzo ya amani nchini Marekani mwezi uliopita.

Maofisa wanasema,wanamtarajia Bw Abbas, kwa mara nyingine tena kuishinikiza Israel kukomesha shughuli zote za makazi katika ardhi inayokaliwa ya Palestina, huku Olmert anatazamiwa kushikilia msimamo wa kuwa pande mbili zimulike mkataba badala ya mikingamo.

Msemaji wa Abbas- Nabil Abu Rudeina,ameliambia shirika la habari la kifaransa-AFP- kuwa mkutano utamulika haja ya kusimamisha ujenzi wa makazi katika eneo la Palestina, na kuongeza kuwa –hadi sasa majadiliano yamekwama kutokana na Israel.

Kiongozi wa tume ya Palestina katika mazungumzo ya amani Saeb Erekat nae amegusia hilo.

Yeye msemaji wa serikali ya Israel-Mark Regev amesema kuwa lengo la mkutano ni kujaribu kuziba pengo lilioko.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice,aliwasiliana na viongozi hao wawili kaktaika mkesha wa leo akiwataka wakutane waondoe vizingiti vya mazungumzo.

Msemaji wa rais Abbas ameongeza kuwa Bw Abbas alimhimiza Bi Rice kuishawishi Israel kukomesha sera yake ya ujenzi wa makazi ambacho alisema ni kizingiti cha mazungumzo ya amani.

Hata hivyo maofisa wa Israel wamekataa kutoa kauli kuhusiana na yaliyokuwa katika simu ya Olmert na Bi Rice.

Bw Abbas amesema kuwa kukwama kwa mazungumzo yaliyofufuliwa nchini Marekani kunatokana na hatua ya Israel ya kuendelea kujenga katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa nguvu na Israel.

Tangu mazungumzo ya Annapolis-Marekani –kumetolewa matangazomawili ya Israel kupanua makazi mashariki mwa Jerusalem pamoja na maeneo yanayokaliwa ya West Bank.

Miongoni mwa makazi yaliyotangazwa kupanuliwa ni lile la Har- Homa mbalo kwa waPalestina linajulikana kama Jebel Abu Ghneim. Kaskazini mwa Bethlehem na kusini mwa mstari wa kijani, ambao uliwekwa baada ya vita vya mwaka wa 1948 kati ya Israel na waaraba.

Israel kwa upande wake haichukulii mradi wa Har Homa kama makazi ikihoji kuwa uko katika mipaka iliopanuliwa ya manispaa ya Jerusalem iliowekwa na Israel baada ya kuuteka na kuuchukua kutoka kwa warabu mnamo mwaka wa 1967.

Hata hivyo jamii ya kimataifa haijatambua upanuzi huo, na waPalestina wamekuwa wakidai kuwa upande wa mashariki wa jerusalem uwe makao makuu ya serikali yao ya hapo baadae.

Jamii ya kimataifa inayachukulia makazi yote kama makazi haramu.