1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wahutubia Umoja wa Mataifa

23 Septemba 2011

Viongozi mbalimbalai wameendelea kuhutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja mjini New York.

https://p.dw.com/p/12fA4
Rais wa mamlaka ya ndani ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas katika Umoja wa MataifaPicha: dapd

Akihutubia kwa mara ya kwanza katika kikao hicho Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema Umoja wa Mataifa unawajibika kudhihirisha kuwa mataifa siyo tu yanaungana katika kulaani, bali yanaungana kivitendo.

Pia amesema upepo wa mageuzi unaovuma katika mataifa ya kiarabu, ni nafasi muhimu katika kuonesha njia mpya ya kushirikiana.

Katika kikao hicho hapo jana Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliishutumu mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya The Hague kwa kuufumbia macho uhalifu unaofanywa na viongozi wa mataifa ya magharibi.

Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 87 aliwaambia viongozi wa dunia kuwa mahakama hiyo haishemiki barani Afrika.

Amesema viongozi kama Rais wa zamani wa Marekani George W Bush na Waziri Muu wa zamani wa Uingereza Tony Blair wamefanya makosa ya uhalifu , lakini mahakama hiyo imewafumbia macho, na badala yake imekuwa ikiwaandamana wale wanaotuhumiwa kutoka mataifa yanayoendelea wengi wao wakiwa ni kutoka Afrika.

Ikumbukwe ya kwamba mahakama hiyo ya The Hague imekwishatoa waranti wa kukakamatwa kwa Rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir ikimuhusisha na mauaji ya halaiki ya Darfur.

Rais Mugabe pia ameinyooshea kidole NATO kwa mashambulio yake nchini Libya na kusema huo ni uhalifu.

Naye Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania akihutubia katika kikao hicho alisema nchi yake inaunga mkono dhamira ya Palestina kutaka kupewa uanachama na pia kutaka vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe

Baadaye hii leo Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahamoud Abbas anatarajiwa kuwasilisha ombi la uanachama kamili wa taifa lake katika umoja huo.

Pembezoni mwa kikao hicho cha Baraza Kuu la Umoja wa mataifa kunafanyika mkutano wa kimataifa kuhusiana na ubaguzi, ambapo akihutubia mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyataka mataifa kutotumia kauli zinazoinesha Israel kuwa taifa la kibaguzi.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Ron Prosor aliushutumu Umoja wa Mataifa kwa kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo na kutoa nafasi kwa wazungumzaji kutoka sehemu mbalimbali kama vile Iran ambayo Rais wake Ahmednejad amekuwa akisisitiza haja ya kufutwa kwa taifa la Israel.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP/ZPR

Mhariri:Josephat Charo