1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Chama tawala Zimbabwe, kukutana kesho.

Nyanza, Halima3 Aprili 2008

Wakati chama tawala nchini Zimbabwe kikiwa tayari kwa duru la pili la uchaguzi, iwapo hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja, Halmashauri kuu ya chama hicho inakutana kesho, kuzungumzia uchaguzi mkuu huo. uliofanyika.

https://p.dw.com/p/DbWR
Viongozi wa Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe, ambao wanasubiriwa kukamilisha kutoa matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini humo.Picha: picture-alliance/ dpa

Kikao hicho cha halmashauri kuu ya ZANU PF, kitajadili mambo mbalimbali kuhusiana na uchaguzi huo ikiwemo kuchunguza makosa yaliyojitokeza.

Chanzo cha habari ndani ya chama hicho, kimesema wajumbe 49 wa Halmashauri kuu wa chama hicho tawala cha ZANU PF, ambao wengi ni viongozi waandamizi wa chama hicho, wanakutana kesho ijumaa katika mkutano huo ulioelezwa kuwa muhimu kabisa.

Kikao hicho kitafanyika wakati ZANU PF, ikiwa tayari kwa duru ya pili ya uchaguzi huo ambapo pia vyombo vya habari vya serikali vikiripoti kurudiwa kwa uchaguzi huo kati ya Rais Mugabe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai, kutokana na kudai kutopatikana kwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi iliyopita, msemaji wa serikali ya nchi hiyo anasema Rais Mugabe yuko tayari kwa kinyang'anyiro hicho cha awamu ya pili.

Wakati chama tawala kikiwa tayari kuingia katika awamu ya pili ya uchaguzi, juhudi za wanadiplomasia wa Kiafrika za usuluhishi kati ya Rais Mugabe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai zimejitokeza, baada ya Rais wa zamani wa Sierra Leone Ahmed Tejan Kabbah kukutana na viongozi hao wawili wanaopingana.

Rais huyo mstaafu mstaafu mbaye aliongoza ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika amesema Rais Mugabe ameonekana kuwa shwari wakati wa mazungumzo yao na anamatumaini kuwa matatizo yanayoikabili nchi hiyo yatatatuliwa kwa amani.

Rais Robert Mugabe, leo alionekana hadharani wakati alipokutana na waangalizi wa uchaguzi huo, ikiwa ni siku ya kwanza tangu alipopiga kura yake, siku ya Jumamosi.

Awali Bwana Kabbah pia alikutana na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha MDC, lakini hakuelezea zaidi mazungumzo yao.

Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote rasmi kuhusiana na matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais baada ya siku tano kupita toka zoezi la upigaji kura kufanyika.

Licha ya chama chake kudai ushindi, kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai anaonekana kujiepusha mwenyewe kujitangaza urais, hatua ambayo inaonekana kujaribu kuzuia vurugu miongoni mwa wafuasi wake.

Kutokana na ukimya wa tume ya uchaguzi katika kutangaza matokeo hayo, chama cha upinzani cha MDC jana kiliamua kutangaza matokeo yake yaliyoonesha kuwa Tsvangirai ameshinda kwa asilimia 50.2 na Mugabe kupata asilimia 43.8 ya kura zilizopigwa.

Katika hatua nyingine Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa Boniface Chidyausiku ametaka watu kuwa na uvumilivu kwa kusema kuwa Tume ya uchaguzi nchini humo inahitaji muda kutoa matokeo ya kura yaliyo sahihi.

Amesisitiza kuwa ni ngumu kupatikana matokeo ya mara moja kutokana na kufanyika chaguzi nne siku moja na kukatolewa picha sahihi kwa watu.

Ameongoza kuwa watu wanapaswa kuwa na subira.

Aidha balozi huyo wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa amekanusha madai yaliyotolewa kwamba uchaguzi huo uliendeshwa kwa hila.

Polisi nchini humo wamekuwa katika tahadhari kubwa katika kuangalia hali ya usalama.

Awali Tume ya uchaguzi nchini humo ilitangaza chama cha upinzani cha MDC kupata viti 109 dhidi ya chama tawala cha ZANU PF waliopata viti 97.

Wakati hayo yakiendelea Zimbabwe badi inakabiliwa na matatizo makubwa kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa idadi kubwa ya wananchi wake na uhaba wa chakula, huku ikiwa imewekewa vikwazo vya uchumi na nchi za magharibi.