1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa BRICS washindwa kukubaliana

MjahidA27 Machi 2013

Viongozi wa kundi la nchi zinazoinukia kuwa nguvu ya kiuchumi, leo wameshindwa kukubaliana juu ya pendekezo la kuwa na benki mpya iliotarajiwa kutoa ushindani kwa benki ya dunia inayodhaminiwa na nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/1856O
Viongozi wa BRICS
Viongozi wa BRICSPicha: Reuters

Baada ya kuwa na mazungumzo katika mkutano wa BRICS uliomalizika mjini Durban Afrika kusini, viongozi hao wamesema bado kuna majadiliano zaidi ambayo yanahitajika katika kufanikisha mpango huo.

Viongozi wa nchi hizo zinazounda kundi la BRICS yani Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, wamesema wamekubaliana juu ya wazo la kuwa na benki itakayokuwa na uwezo wa kuyasaidia mataifa hayo kiuchumi lakini ni lazima kuwe na mazungumzo zaidi ya kufanikisha wazo hilo.

Mwenyeji wa mkutano huo rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema wameridhika kuwa kuna matumaini ya kuunda benki hiyo. Matamshi yake yanalenga hatua chache zilizopigwa baada ya mkutano uliofanyika New Delhi mwaka mmoja uliopita.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: Stringer/AFP/Getty Images

Hata hivyo Zuma amesema kwa sasa wamekubaliana kufanya majadiliano mengine ya kina ili kufanikiwa kuunda benki hiyo.

Mawaziri wa Fedha kukutana

Mawaziri wa fedha kutoka nchi hizo tano ambao wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa muda wa mwaka mmoja uliopita sasa watalazimika kuingia katika majadiliano zaidi ya kuja na mikakati kabambe ya kuendeleza mpango wa kuunda benki hiyo.

Kulingana na wanadiplomasia, kundi la BRICS liliazimia kuzindua mpango huo unaohitaji Euro bilioni 50 lakini swala la fedha zitakazochangia kila nchi, miradi itakayoendeshwa na fedha hizo na ni wapi benki hiyo itakapowekwa ni kati ya mambo ambayo yametoa changamoto kubwa katika kuunda benki ya kujitegemea ya kundi hilo.

Viongozi wa kundi la BRICS
Viongozi wa kundi la BRICSPicha: picture-alliance/dpa

Kwa sasa ni vigumu kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho kila nchi itachangia haswaa baada ya Rais Jacob Zuma kusema kuwa kiwango kitakachotolewa kinapaswa kuwa kiwango ambacho kitaiwezesha benki hiyo kufanya kazi kwa uthabiti.

Akizungumza na shirika la habari la AFP mjumbe wa Urusi aliyeko Afrika Mikhail Margelov amesema ni muhimu kuzungumzia kuhusu miradi itakayoendeshwa na benki hiyo mwanzo badala ya kuanza kujikita katika maswala ya fedha.

Hata hivyo katika mkutano huo uliomalizika hii leo kuna maswala mengine ambayo yamefanikishwa kama kuzinduliwa kwa mkutano wa kibiashara kwa mataifa hayo matano ambao utasaidia katika uekezaji na kuinua biashara katika masoko yanayoinukia.

Waziri wa fedha wa Brazil Guido Mantega na mwenzake wa China Lou Jiwei
Waziri wa fedha wa Brazil Guido Mantega na mwenzake wa China Lou JiweiPicha: Reuters

Katika mkutano huo pia mikataba kadhaa ya bishara yalitiwa saini ikiwemo ule kati ya Brazil na China waliokubaliana kufanya biashara pamoja.

Mwandishi Amina Abubakar AFP/ dpa
Mhariri Yusuf Saumu