1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi na wanasiasa wamuenzi Helmut Kohl

Sekione Kitojo
17 Juni 2017

Kansela wa zamani  wa Ujerumani  Helmut Kohl, msanifu wa muungano wa Ujerumani mbili  na mwanasiasa mwenye ushawishi  mkubwa katika karne iliyopita, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87 Ijumaa(16.06.2017).

https://p.dw.com/p/2eqm6
Helmut Kohl Buchvorstellung Vom Mauerfall zur Wiedervereinigung
Picha: Getty Images/H. Foerster

Kansela  Angeöla  Merkel  aliwaambia  waandishi  habari wakati  akiwa  katika  ziarani  mjini Rome kwamba Kohl ameonesha "uzalendo  wa  hali  ya  juu  katika kuwahudumia  wananchi  pamoja  na  amani."

"Helmut Kohl kwa hiyo amekuwa mwale wa  bahati kwetu sisi Wajerumani," amesema.

"Binafsi nafarijika  kwamba  alikuwapo," Merkel  aliongeza, akisisitiza  jukumu  alilokuwa  nalo  katika  kumsaidia kuingia  katika  siasa  za  mstari  wa  mbele. Kohl aliiongoza  Ujerumani  katika  muungano  mwaka  1990  na alikuwa  kansela  wa  Ujerumani  ya  magharibi  kuanzia mwaka  1982 hadi 1998  na  kisha  taifa  la  Ujerumani lililoungana .

Tangu  pale  alipoanguka  na  kupata  athari  katika ubongo  mwaka  2008, Kohl amekuwa  mgonjwa  sana, hali yake  ikiporomoka  kwa  kiasi  kikubwa. Alikuwa  yuko katika  nyumba  yake  tu  mjini  Ludwigshafen, ambako alitembelewa  mwezi  Aprili  2016 na  waziri  mkuu  wa hungary Viktor Orban .

Alifariki  akiwa  nyumbani  kwake.

Deutschland | CDU-Parteitag in Dresden 1991
Kansela wa wakati huo Helmut Kohl akiwa na kansela wa baadae Angela Merkel, wakati huo akiwa waziri wa masuala ya wanawake, katika mkutano mkuu wa chama cha CDU mjini Dresden, Desemba 16. 1991.Picha: picture-alliance/ dpa/dpaweb

Viongozi  mbali  mbali  duniani , viongozi  wa  zamani na wanasiasa  walielezea  hisia  zao  kutokana  na  kifo  cha Helmut Kohl  jana  Ijumaa  mara  baada  ya  taarifa  za  kifo chake  kupatikana.

Rais  wa  zamani  wa  Marekani  George HW  Bush amesema " Wajerumani  walimpa  Helmut Kohl  jina  la utani "Kansela  wa  muungano." Hii  ni  sahihi  na muafaka."

Viongozi watoa maelezo kuhusu Kohl

"Alitakiwa  kujibu  baadhi  ya  maswali  mazito  katika wakati  wake, na  katika  kujibu kwa  usahihi  aliwezesha muungano  wa Ujerumani  iliyokuwa  imara, yenye ufanisi na  kuundwa  kwa  Umoja  wa  Ulaya."

"Msanifu wa  muungano  wa  Ujerumani  na  urafiki  kati  ya Ujerumani  na  Ufaransa: kwa  kifo  cha  Helmut Kohl , tumempoteza mtu  muhimu  sana  katika  Ulaya." amesema rais  wa  Urusi Vladimir Putin.

Rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron  amesema, "Ni Mjerumani  halisi na  juu  ya  yote  amefariki  mtu  halisi  wa Ulaya."

Katibu  mkuu  wa  NATO Jens Stoltenberg , amesema "Kifo cha  Helmut  kinaniumiza  sana. Mtu ninayejifunza  kwake, rafiki  wangu, mwenye  uhalisia  wa  Ulaya, atakumbukwa sana, na  tutamkosa sana."

Helmut Kohl und Wladimir Putin
Helmut Kohl akiwa na rais wa Urusi Vladmir Putin katika makaazi ya Putin yalioko Novo-Ogaryovo nje ya mji mkuu wa Urusi, Moscow, Oktoba 13, 2005.Picha: picture-alliance/dpa

"Helmut Kohl  alikuwa  sehemu  ya  Ujerumani  iliyoungana katika  Ulaya  iliyoungana. Wakati  ukuta  wa  Berlin ulipoanguka , alijitokeza  juu  kabisa. Mtu halisi  wa  Ulaya." Amesema  waziri  wa  mambi  ya   kigeni  wa  Ujerumani Sigmar Gabriel.

"Helmut  alikuwa historia  kubwa  ya  Ulaya. Alihakikisha muungano  wa  furaha kwa  nchi  yake  na  kusaidia  ujenzi wa  Ulaya na  uhuru."

Waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Uingereza Boris Johnson amesema, "Kalale  mahali  pema  Helmut Kohl, mtu mwenye  maono  katika  Ulaya  na  kiongozi  wa  dunia. Katika  enzi  za  kuongezeka  kwa  hali  ya  kujitenga tunaweza  kujifunza  mengi  kutokana  na  mfanyo  wame wa  muungano."

Waziri  mkuu  wa  Uingereza Theresa  May  amesema, "kama kansela  wa  kwanza wa  Ujerumani  iliyoungana tangu  mwaka  1945 alikuwa  kinara  wa  historia  ya  ulaya. Kwa  niaba  ya  watu  wa  Uingereza natoa hongera  kwa jukumu  alilochukua  katika  kusaidia  kumaliza  vita  baridi na  kuziunganisha  Ujerumani  mbili. Tumempoteza baba wa  Ujerumani  ya  kisasa.

Waziri  mkuu  wa  Italia Paolo Gentiloni  amesema , Heko kwa  kumbukumbu ya  kansela Kohl. italia  inamkumbuka kama muasisi  wa  muungano  wa  Ujerumani  na kuanguka  kwa  ukuta  katika  bara  la  Ulaya."