1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Urusi vaamriwa na Kremlin virejee kambini

19 Mei 2014

Urusi imewaamuru wanajeshi wake waliowekwa karibu na mpaka wa Ukraine warejee kambini, hatua inayodhihirisha azma ya kutaka kutuliza hali ya mambo, wiki moja kabla ya uchaguzi wa kabla ya wakati wa rais nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/1C2da
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Alexey Nikolsky/AFP/Getty Images

"Vladimir Putin ameitaka wizara ya ulinzi iwarejeshe wanajeshi kambini kutokana na kumalizika mazowezi yaliyowalazimisha kuhamishiwa katika maeneo ya Rostov,Belgorod na Briansk,karibu na Ukraine.

Wakati huo huo rais Vladimir Putin ameitolea mwito Ukraine pia isitishe kile alichokiiita "opereshini ya ukandamizaji na ya matumizi ya nguvu" akimaanisha opereshini dhidi ya magaidi inayoendeshwa na jeshi la Ukraine.

Taarifa ya Kremlin imetolewa katika wakati ambapo maeneo yaliyojitenga ya Lugansk na Donetsk,mashariki ya Ukraine bado yanasumbuliwa na mapigano ya hapa na pale kati ya makundi ya waasi na wanajeshi wa Ukraine.

Hakuna dalili ya kurejea nyuma wanajeshi wa Urusi

Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen anasema hakuna ishara yoyote ya kuanza kurejea nyuma wanajeshi wa Urusi.

Rasmussen in Warschau 08.05.2014 PK mit Tusk
Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh RasmussenPicha: Reuters

Waziri wa ulinzi wa Ukraine ametangaza kifo cha mwanajeshi mmoja hii leo aliyeuliwa kufuatia shambulio la waasi karibu na Slaviansk-ngome ya waasi inayozingirwa na vikosi vya serikali.

Matumizi ya nguvu yaliyoagamiza maisha ya karibu watu 130 tangu opereshini dhidi ya magaidi ilipoanzishwa ,april 13 iliyopita,yanahofiwa yasije yakakarofisha zoezi la uchaguzi katika majimbo la Lugansk na Donetsk.

Kwa mujibu wa ripoti zilizolifikia shirika la habari la Ufaransa AFP kutoka tume ya uchaguzi,watu milioni mbili wanakabiliwa na hatari ya kutoweza kupiga kura au kulazimika kupitisha masaa kadhaa kuweza kwenda kupiga kura katika mojawapo ya vituo vinavyodhibitiwa na serikali.

"Katika baadhi ya maeneo ya maashariki,itakuwa shida kuandaa uchaguzi" amekiri waziri mkuu Arsenyi Yatsenyuk alipokutana na magavana wa majimbo.Hata hivyo amehakikisha uchaguzi utafanyika na rais wa halali atachaguliwa-anasema.

Wapinzani wa Kiev watapata shida kuutia ila uchaguzi

Mpatanishi wa jumuia ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE,mwanadiplomasia wa Ujerumani Wolfgang Ischinger anaamini pia uchaguzi utafanyika jumapili ijayo,ila katika baadhi ya maeneo ya mashariki-karibu asili mia 10 ya miji ya eneo hilo anahofia itakuwa shida.Akizungumza na kituo cha matangazo cha Deutschlandfunk,bwana Ischinger anasema matokeo ya uchaguzi yatawapa shida wapinzani wa serikali ya mjini Kiev kuudai uchaguzi huo haukuwa halali.

Gespräche in Charkiw
Mwakilishi wa jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya Wolfgang Ischinger (kulia)Picha: DW/O.Indukhowa

Wagombea wakuu wa kiti cha rais wanaendelea na kampeni zao na hakuna,yeyote,mbali na waziri mkuu wa zamani Yulia Timoschenko aliyezungumza na waandishi habari mjini Donetsk,mwezi uliopita,,aliyeutia mguu wake hadi sasa katika miji ya Donetsk na Lougansk.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman