1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya serikali ya mpito vyashambulia Sirte

20 Oktoba 2011

Wapiganaji wa uongozi wa mpito nchini Libya leo hii wameanza operesheni nyingine ya mashambulizi dhidi ya ngome ya mwisho ya kiongozi aliye mafichoni, Muammar Gaddafi, katika mji waliouzingira wa Sirte

https://p.dw.com/p/12vma
Mashambulizi mjini SirtePicha: picture-alliance/dpa

Duru zinaeleza kuwa zana za kivita kama maroketi na vifaru zimeonekana zikielekea katikati ya mji huo ulio katika ukanda wa pwani.

Mtangazaji wa televisheni ya Al Jazeera ameoneshwa akisema zana hizo zilikuwa zikielekea katikati mwa mji wa Sirte mapema asubuhi. Mpiganaji mmoja amenukuliwa akimwambia mtangazaji wa kituo cha Al Arabiya kwamba hivi sasa wanakabiliana na watunguaji, ambao wamejificha katika maeneo ya mji huo.

Bwana huyo aliendelea kusema wanajitahidi kukwepa kutumia vifaru na maroketi ili kuepusha madhara zaidi kwa raia wasio na hatia kwa sababu maeneo wanayokusudia yana wakaazi wengi.

Kriegsfront in Bani Walid Libyen Flash-Galerie
Wapiganaji wa uongozi wa mpitoPicha: Essam Zuber

Mamia ya vikosi vya Baraza la Mpito la Uongozi wa Libya yamekuwa wakipambana kuudhibiti mji wa Sirte, ambako ndiko alikozaliwa Gaddafi. Wiki iliyopita walisalimu amri kutoka katika baadhi ya maeneo ya mji huo, baada ya kushambuliwa na askari watiifu kwa kiongozi huyo.

Jumatatu wapiganaji hao walifanikiwa kuuweka kizuizini mji mwingine wa Bani Walid baada ya mapigano makali ya takribani miezi miwili, eneo ambalo pia lilikuwa ngome ya kiongozi huyo wa zamani wa Libya.

Kama wapiganaji hao watafanikiwa kuuweka katika himaya yao mji wa Sirte basi uongozi mpya wa nchi hiyo utakuwa umekamilisha mchakato wa kudhibiti eneo lote la Libya, tangu kuondolewa madarakani kwa Gaddafi na kuufikisha kikomo utawalawa wake wa miaka 42.

Wakati hayo yakienndelea kiongozi namba mbili wa serikali ya mpito ya Libya, Mahmud Jibril, ameonya kutokea vitendo vya kuvuruga amani nchini humo kabla ya kukamilika kwa mchakato wa ukombozi kamili wa taifa hilo.

Jibril ambaye aliwahi kuwa afisa mwandamizi katika masuala ya uchumi wakati wa serikali ya Gaddafi amesema hatua hiyo itaweza kusababishwa na mgogoro wa kuwania madaraka miongoni mwao.

Akizungumza katika mkutano wake na waliokuwa wapiganaji waasi kwa lengo la kustawisha taifa lenye utawala wa sheria alisema taifa hilo limeingia katika vita vya kisiasa hata kabla ya ukombozi wake haujakamilika.

Mkutano huo umefanyika huku kukiwa na shaka kwamba kumalizika kwa utawala wa Gaddafi kutafuatiwa na mgawanyiko wa makundi mbalimbali wakiwemo waislamu wenye msimamo mkali, wa kati pamoja na vikundi vya kikabila vyenye mitazamo tofauti.

Akizungumza na jarida lilitwalo Time alisisitiza azma yake ya kujenga Libya iliyo bora na yenye misingi ya kidemokrasia huku akisema yupo tayari kuondoka katika wadhfa wake ili kuacha vyama vya kiraia na taasisi nyingine kufanikisha hatua hiyo.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/DPAE
Mhariri:Josephat Charo