1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi

Yusra Buwayhid
23 Septemba 2019

Kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi Jumatatu, vijana wameandamana mjini New York. Ujumbe wao kwa viongozi wa dunia ni kwamba hali kwa sasa ni ya dharura.

https://p.dw.com/p/3Q4ol
USA Globaler Klimastreik | New York | Greta Thunberg
Picha: Getty Images/D. Angerer

Katika kipindi cha miaka miwili na nusu tangu kuingia madarakani, Rais wa Marekani Donald Trump amefuta sheria kadhaa za kulinda mazingira na kuiondoa nchi yake katika mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ulioafikiwa mjini Paris, ambao unalenga kuzuia ongezeko la joto ulimwenguni lisizidi nyuzi joto mbili. Kutokana na historia yake hiyo, Marekani sio nchi muafaka kuwa mwenyeji wa mkutano unaohusu mabadiliko ya tabianchi. Lakini Umoja wa Mataifa Jumatatu ndiyo utafungua mkutano huo wa kielele, katika makao yake makuu mjini New York.

Ni mkutano utakaojaribu kuanzisha kampeni ya kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Katika vikao viwili, takriban viongozi wa dunia wapatao 60 watatangaza hatua wanazopanga kuchukua kupambana na ongezeko la joto ulimwenguni. Miongoni mwa viongozi watakaozungumza, ni Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi. Umoja wa Mataifa umeamua kuwanyima nafasi ya kuzungumza viongozi wa mataifa ambayo hayafanyi vya kutosha kutimiza malengo yaliyowekwa wakati wa Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi ya mjini Paris. Soma zaidi: Kilio cha vijana wa dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

USA Greta Thunberg in NewYorkGreta Thunberg deltar på FN klimat toppmöte för unga i...
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anthonio Guterres akipeana mkono na mwanaharakati Greta Thunberg.Picha: picture-alliance/TT NYHETSBYRÅN/P. Lundahl

Akizungumza na waandishi habari mnamo mwezi Agosti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amewaambia viongozi wa dunia wasije katika mkutano huo na hotuba za kupendeza, bali waje na mipango halisi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Guterres alikutana pia na wanaharakati hao vijana na kukiri makosa ya kizazi cha umri wake:

"Kizazi cha umri wangu kimeshindwa hadi sasa kulinda haki za binadamu pamoja na kuuhifadhi ulimwengu. Nina wajukuuu. Nataka wajukuu wangu waishi katika dunia inayoeleweka. Kizazi cha watu wa umri wangu kina jukumu kubwa. Na kizazi chenu lazima kituwajibishe kuhakikisha hatusaliti musatakbali wa wanadamu," amesema Guterres.

Wakati Rais Trump hatohudhuria mkutano huo wa Jumatatu, afisa wa ngazi ya juu wa Merekani na ujumbe maalumu anatarajiwa kushiriki. Hakijulikani watakachosema, lakini wataalamu wanasema kutokana na ongezeko la joto - na kuongezeka kwa sauti za wanaharakati vijana wanaopigania suala la mabadiliko ya tabianchi nchini Marekani- wakati wa kukataa kuwepo kwa tatizo hilo umeshapita.

Msimamo huo uliakisiwa katika Mkutano wa Kilele wa Vijana uliofanywa makao makuu ya Umoja wa Mataifa Jumamosi iliyopita, ambapo zaidi ya vijana 1,000 kutoka nchi zipatazo 140 walikutana na kujadili mikakati ya kuyalinda mazingira na kuwashawishi wanasiasa kulichukulia hatua za msingi suala la mabadiliko ya tabianchi.

Source: DW