1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanashitakiwa kwa makosa ya kula njama za kutoa rushwa

21 Novemba 2017

Kwa mara ya pili katika miaka miwili, waendesha mashtaka wa serikali Marekani, wamewasomea mashtaka wafanyabiashara wa kigeni, kwa madai ya kutoa rushwa ya mabilioni ya dola ili kupata fursa za kibiashara.

https://p.dw.com/p/2o00X
USA Gerichtsprozess gegen einen vermeintlichen Unterstützer des IS
Moja ya Mahakama nchini MarekaniPicha: Reuters/S. Stapleton

Sehemu ya rushwa hiyo inadaiwa kwenda kwa aliyekuwa Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa kutoka Uganda. 

Dk Chi  Ping Patric Ho, wa Hong Kong na Cheikh Gadio, wa Senegal, walihukumiwa kwa makosa ya jinai  kwenye mahakama ya Manhattan. Walisomewa mashtaka ya rushwa, utakatishaji fedha wa kimataifa na  njama za kufanya makosa yote hayo.

``Inadaiwa kuwa njama za Uganda zilipangwa mjini New York, katika  ukumbi wa Umoja wa Mataifa, wakati huo, waziri wa sasa wa mambo ya nje, alikuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na uliendelea hadi aliporudi Uganda,`` Amesema Kaimu Wakili wa Marekani, Joon H. Kim katika taarifa yake kuhusu kukamatwa kwao jana.

William F. Sweeney Jr, Mkuu wa Ofisi ya  shirika la upepelezi wa ndani Marekani FBI New York, amesema Gadio na Ho, walitaka kujipatia fursa adhimu za kibiashara  Afrika.

Alisema,  inadaiwa kuwa walikuwa tayari kuwapa fedha viongozi wa nchi hizo mbili (Uganda na Chad)ili kupindisha taratibu za kawaida za kibiashara. Lakini hawakujua kuwa kutumia mfumo wa kibenki wa Marekani,  kutawagharimu.

Angel M. Melendez, Mkuu wa Kitengo cha  Usalama wa nchi New York,  amesema  waliotoa mamilioni hayo ya dola kama rushwa, waliyatoa kwa jina la misaada ya wahisani ili kupata fursa za kibiashara.

Amesema Ho, alitumia  nafasi yake kama mshauri wa kiuchumi wa Umoja wa Mataifa na halmashauri za Jamii,  ili kurahisisha mipango yake ya rushwa.

Wakili wa Ho,Paul Kreiger  alikataa kuzungumza kuhusu suala hilo.

Lakini Wakili wa Gadio, Robert Baum, alisema mteja wake ameshangazwa na mashtaka hayo.

Wakili wa mtuhumiwa azungumza kwa njia ya barua

Akijibu kwa njia ya barua pepe, Baum amesema: ``Gadio amefanya kazi kama Profesa wa Chuo, amefanya kazi katika miradi mbalimbali kwa maslahi ya umma. Amekuwa wakala wa amani Afrika huku akisimamia mapato ya mamilioni ya dola. Uaminifu wake na uadilifu wake,  haujawahi kutiliwa shaka. ``

Infografik Tschad ENG
Ramani ya Taifa la Chad

Watuhumiwa wote walifika mahakamani katika hatua za awali.  Ho anashikiliwa kwa ridhaa ya mawakili wake, wakati Gadio anaendelea kushikiliwa kwa dhamana ya dola milioni moja. 

Mwanzoni mwa Oktoba 2014, waendesha mashtaka walisema Ho na Gadio walipanga kutoa rushwa ili kupata fursa za kibiashara kwenye makao makuu ya  kampuni  kubwa ya kimataifa ya Shanghai inayojihusisha   na masuala ya nishati na sekta ya kifedha.

Imeelezwa kuwa katika moja ya mipango yao, Ho na Gadio walishtakiwa kwa kusababisha kampuni moja ya nishati, kutoa rushwa ya dola milioni 2 kwa Rais wa Chad ili wapate haki muhimu za mafuta kutoka kwa serikali ya Chad, bila kushindanishwa kimataifa.

Katika mpango mwingine, Ho, anadaiwa kuwa chanzo cha  Waziri wa Mambo ya nje wa Uganda, kupewa rushwa ya dola 500,000 muda mfupi baada ya kumaliza muhula wake kama Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.  Waendesha mashtaka wamesema kuwa rushwa hiyo ilitolewa ili kupata fursa za kibiashara katika kampuni ya nishati ambayo hata hivyo haikutajwa mahakamani.

 Mwandishi: Florence Majani(AP)

Mhariri: Saumu Yusuf