1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uvira, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Wanajeshi wa Nkunda waondoka katika jeshi la DRC.

25 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWI

Ghasia miongoni mwa waasi wa zamani wa Kitutsi walioingizwa katika jeshi la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo zinatishia kusitisha miezi minane ya usitishaji wa mapigano na kulitumbukiza eneo la mashariki ya nchi hiyo katika vita.

Siku ya Alhamis majeshi yanayomuunga mkono jenerali muasi Laurent Nkunda , ambaye aliongoza mapigano ya mwaka 2004 katika eneo la Kivu ya kaskazini akitaka kuwalinda raia wa Kitutsi ambao ni wachache nchini humo, walianza kujitoa katika jeshi bila ya kibali cha viongozi wa juu wa jeshi hilo.

Kamanda wa majeshi ya Kongo katika jimbo la Kivu ya kaskazini , jenerali Vainqueur Mayala , amesema hafahamu uamuzi wowote rasmi wa wanajeshi wanaomuunga mkono Nkunda kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Ujumbe wa umoja wa mataifa wa kulinda amani MONUC , umepeleka majeshi yake huko Kivu ya kaskazini wakati hali ya wasi wasi ikizidi.