1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uungwaji mkono wa Magufuli washuka kwa 41%

Veronica Natalis
5 Julai 2018

Ripoti ya shirika la Twaweza nchini Tanzania inaonyesha kuwa wananchi 6 kati ya 10 wanasema uhuru wa vyama vya upinzani, asasi za kiraia na vyombo vya habari umepungua ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

https://p.dw.com/p/30sa2
Tansania Präsident John Magufuli
Picha: DW/S. Khamis

Ripoti hiyo pia inaonyeaha kuwa wananchi 9 kati ya 10 bado wanapendelea demokrasia ya vyama vingi. Ripoti hiyo inasema, wanapotathmini viashiria mbalimbali vya demokrasia, wananchi wengi, wanasema uhuru umepungua katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Asilimia 64 ya waliohojiwa wanasema uhuru umepungua kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutoa maoni yao, asilimia 62 wanasema uhuru wa vyombo vya habari kukosoa au kuripoti maovu ya serikali umepungua, na makundi yasiyofungamana na upande wowote kupaza sauti zao na kufanya mikutano kwa asilimia 58.

Ni utafiri wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye tatifi zake mbili ziitwazo: "Nahodha wa meli yetu wenyewe?" na "Tuwapashe Viongozi?". Tafiti hizi zinatokana na takwimu kutoka "Sauti za Wananchi", utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.

Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,241 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara mwezi Aprili mwaka 2018. Zanzibar haikuhusishwa  kwenye utafiti huu.

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze
Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan EyakuzePicha: DW/S. Khamis

Wananchi wanataka uwazi zaidi kwenye uwajibikaji ambapo asilimia 59 ya wananchi wanataka Rais awajibishwe na Bunge kutoa maelezo ya matumizi ya fedha za walipa kodi, na wananchi wengi zaidi.

Asilimia 78 ya wananchi wanataka Rais aheshimu sheria na maamuzi ya mahakama. Uungaji mkono wa haki za vyama vya upinzani nao pia umeongezeka. Asilimia 37 ya wananchi wanasema vyama vya upinzani vinapaswa kuikosoa na kuifuatilia serikali ili kuiwajibisha mara baada ya vipindi vya chaguzi kuisha ukilinganisha na asilimia 20 tu walisema hivyo mwaka 2016.

Na wananchi wengi zaidi wanasema vyama vya upinzani viruhusiwe kufanya mikutano mwaka huu  ukilinganisha na mwaka 2016 Kuhusu suala la kukataza maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani, wananchi 5 kati ya 10 wanapinga katazo hilo huku 4 kati ya 10 wakiunga mkono.

Wananchi bado wanawaunga mkono wagombea wa CCM

Kwa upande wa Rais uungwaji mkono umeserereka kutoka 96% mwaka 2016, ambavyo vilikuwa ni viwango vya juu kuwahi kutokea nchini, mpaka 55% mwaka 2018, viwango vya chini kabisa kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi.

Pamoja na hilo, wananchi kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuwaunga mkono wagombea wa CCM. Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: "Wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa kanuni za kidemokrasia japokuwa wanaona zipo mashakani."

Mwandishi: Veronica Natalis

Mhariri: Iddi Ssessanga