Uturuki yatishia kushambulia Wakurd | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 12.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Uturuki yatishia kushambulia Wakurd

Uhusiano kati ya Marekani na mshirika wake wa desturi Uturuki umepoza,baada ya tume ya wabunge wa Marekani iliyoundwa na wizara ya nje kueleza kuwa kulitokea mauaji ya halaiki,Waarmenia walipofukuzwa kwa nguvu kutoka Anatolia,wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza-jambo linalopingwa na serikali ya Uturuki.

Uamuzi wa tume hiyo ya wabunge wala haushangazi, kwani tangu miongo kadhaa hilo lilikuwa lengo la kundi dogo la washawishi wa Kiarmenia ambao wana usemi,nchini Marekani.Kwa muda mrefu Bunge la Marekani lilizuia uamuzi wa aina hiyo kwa sababu Uturuki ni miongoni mwa washirika muhimu kabisa wa Marekani.Serikali ya Ankara,huiruhusu Marekani kutumia anga yake kupitisha vikosi na mahitaji ya vikosi hivyo hadi Irak na Afghanistan.

Lakini tangu mwanzoni mwa mwaka huu,baada ya bunge kudhibitiwa na Wademokrat,wabunge wa majimbo yenye wakaazi wengi wenye asili ya Kiarmenia kama vile California,New Jersey na Michigan,wameifufua mada hiyo.Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani,Bibi Nancy Pelosi alipoulizwa kwanini uamuzi huo umepitishwa wakati huu alijibu kuwakamwe hakuna wakati muwafaka. Hata hivyo amesema,viongozi wa chama cha Demokratik wanaunga mkono kutambua mauaji hayo kama mauaji ya halaiki.

Kwa upande mwingine,Uturuki,imemwita nyumbani balozi wake kutoka Washington na imeonya kuwa kutakuwepo athari kubwa,ikiwa Bunge la Marekani pia litaita mauaji ya Waarmenia yaliyofanywa na Waturuki karne moja iliyopita,mauaji ya halaiki. Egeman Bagis,alie mshauri wa Waziri Mkuu wa Uturuki,Recep Tayyip Erdogan alipozungumza na waandishi wa habari mjini Ankara alisema,Uturuki huenda ikalazimika kukatisha msaada wake wa miundombinu kwa Marekani.

Washington ilielewa tangu hapo awali vipi uamuzi wa kueleza mauaji hayo kama mauaji ya halaiki,utakavyopokewa na Uturuki.Kwani hapo kabla,Rais George W.Bush na hata mawaziri wa ulinzi Robert Gates na wa nje,Condoleezza Rice walionya kuwa uamuzi wa aina hiyo utamhamakisha sana mshirika wao.

Wachambuzi wa kisiasa wamesema,uamuzi wa tume ya wabunge,huenda ukaichochea zaidi Uturuki kupeleka vikosi vyake kaskazini mwa Irak,kuwasaka waasi wa Kikurd-hatua inayopingwa vikali na Marekani,kwani hatua hiyo,itazusha machafuko katika eneo lenye utulivu wa aina fulani nchini Irak.

Waziri Mkuu Erdogan hii leo amesema,serikali yake ipo tayari kukabiliana na lawama za kimataifa na ipo tayari kukabiliana na hasara yo yote ile.

Marekani na Umoja wa Ulaya ambamo Uturuki ingependa kuwa mwanachama,zimieonya Ankara kutowashambulia Wakurd,kaskazini mwa Irak.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com