1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tupewe pasi huru au tuachane na mpango wa wakimbizi

Mjahida 15 Agosti 2016

Uturuki inasema Umoja wa Ulaya unapaswa kutoa kibali cha pasi huru za kusafiria kwa raia wa nchi yake ifikapo Oktoba 2016 au mpango wa wahamiaji unaojumuisha Uturuki kuzuia wimbi la wakimbizi kuingia Ulaya uwekwe kando.

https://p.dw.com/p/1JiQk
Türkei Aussenminister Mevlut Cavusoglu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut CavusogluPicha: picture alliance/AP Photo/A. Unal

Akizungumza na gazeti la Jumapili la Bild la nchini Ujerumani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alisema Ulaya inapaswa kuchagua moja kati ya mawili hayo.

Alipoulizwa iwapo maelfu ya wakimbizi walioko Uturuki wataachiwa waingie Ulaya ikiwa Umoja huo hautaridhia matakwa ya Uturuki ifikapo mwezi Oktoba, Cavusoglu alisema hataki kuzungumzia mazingira hayo mabaya. "Mazungumzo kati ya Uturuki na Umoja huo yanaendelea lakini ni wazi kuwa ama mikataba yote itumike kwa wakati mmoja au iwekwe kando", alisema.

Kupata pasi huru ya kuingia barani Ulaya ni moja ya 'zawadi' inayotaka Uturuki baada ya kukubali kuzuwiya mmiminiko wa wakimbizi wanaotaka kuingia barani humo. Lakini mpango huo umekuwa ukicheleweshwa kufuatia kile Ulaya inachosema ni mzozo juu ya sheria ya Uturuki ya kupambana na ugaidi na msako unaofanywa sasa na serikali ya nchi hiyo, baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

Türkei Erdogan in Ankara
Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AA/G. Yilmaz

Kabla ya ombi la Uturuki kuzingatiwa, Umoja wa Ulaya unaitaka kwanza ilegeze sheria yake dhidi ya ugaidi. Kamishna wa Umoja wa Ulaya, Guenther Oettinger, anaamini kuwa Umoja huo hautaliridhia ombi hilo la Uturuki kwa mwaka huu, kutokana na namna serikali mjini Ankara inavyoendesha msako wake baada ya jaribio hilo la mapinduzi la katikati ya mwezi Julai.

Kwa upande wake, Cavusoglu alisema mikataba iliyopo inasema raia wote wa Uturuki watapata pasi huru ya kusafiria ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu. "Haiwezekani kutekeleza kila kitu kilicho kizuri kwa Umoja wa Ulaya huku Uturuki ikitoka patupu."

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya hakupatikana kujibu mara moja kuhusu kauli hiyo ya Cavusoglu.

Balozi wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya asema mikakati ya kupata suluhisho inaendelea.

Wiki iliyopita, Balozi wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya, Selim Yenel, alisema mikakati inaendelea kupata suluhisho na Umoja huo juu ya ombi la Uturuki huku akisema kuwa anafikiria hilo litawezekana mwaka huu wa 2016. Balozi Yenel alikanusha kuwa suala hilo linaweza lisitekelezwe mwezi Oktoba baada ya kukosa kutekelezwa pale muda wake wa awali ulipopita mwezi Juni.

Europäisches Parlament Stoppuhr EU-Kommisar für digitale Wirtschaft und Gesellschaft Günther Oettinger
Kamishna wa Umoja wa Ulaya, Guenther OettingerPicha: picture-alliance/dpa/Julien Warnand

Kwa upande wake, Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki alisema angeliidhinisha hukumu ya kifo iwapo bunge lingeupigia kura mswaada huo, hatua ambayo inaonekana kudidimiza matumaini ya nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hukumu hiyo ya kifo inatolewa kwa wale watakaopatikana na makosa ya ugaidi.

"Ulaya inachukua hatua kama kwamba tayari wameshapitisha sheria hiyo ya hukumu ya kifo," alisema Cavusoglu , akiongeza kuwa Rais Erdogan hakutaka sheria hiyo ipitishwe, lakini kumekuwepo na sauti nyingi za unyonge kutoka Uturuki na hilo halikupaswa kupuuziwa.

Kwa upande mwengine, alipoulizwa iwapo watajiondoa katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Cavusoglu alisema makundi yanayoiunga mkono Uturuki yapo katika mazungumzo juu ya hilo lakini akasisitiza kuwa "Uturuki ni moja ya waungaji mkono wakubwa wa jeshi hilo la ulinzi la mataifa 28 ya Magharibi."

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef