1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshikamano si madhubuti Uturuki

8 Agosti 2016

Mapambano dhidi ya wanamgambo wa dola la Kiislam IS,hali nchini Uturuki na hali ya kiuchumi nchini Marekani ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

https://p.dw.com/p/1JdLy
Maandamano ya mjini IstanbulPicha: DW/D. Cupolo

Tunaanzia lakini na juhudi za kuwashinda nguvu wanamgambo wa kundi la kigaidi la dola la Kiislam IS. Gazeti la Hannoversche Allgemeine linajiuliza:"Ushindi katika uwanja wa mapigano dhidi ya IS unasaidia nini ikiwa magaidi wakati huo huo wanafanikiwa kueneza ukatili wao kupitia mshambuliaji mmoja mmoja wanaojitambulisha na kundi hilo la kigaidi? Obama amekumbusha jukumu ambalo mtangulizi wake tayari alilitaja katika mapambano dhidi ya Taliban,bila ya kulitekeleza: Ushindi unabidi uanzie kichawni. Chuki na itikadi kali ya dini ya Kiislam zinabidi ziondolewe vichwani mwa watu,tena kila mahala.

Mshikamano haujakamilika Uturuki

Hali nchini Uturuki inaendelea kugonga vichwa vya habari nchini Ujerumani. Mamilioni walikusanyika jana mjini Istanbul kulaani njama iliyoshindwa ya mapinduzi. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:"Hivyo ndiyyo siku ya suluhu inavyokuwa,ikiwa imeitishwa na chama pekee tawala AKP. Ingawa chama hicho kinachoongozwa na Erdogan kimekataza watu wasipepee bendera za vyama vya kisiasa,ili kutovuruga azma ya kudhihirisha mshikamano wakati wa kongamano hilo mjini Istanbul. Nia hiyo lakini haikufuatwa kikamilifu. Ingawa kujitokeza Erdogan na viongozi wa upinzani Kilicdaroglu na Bahceli ni ushahidi kamili kwamba upande wa upinzani na serikali wanalaani njama ya mapinduzi ya kijeshi. Hata hivyo kwa kutojumuishwa chama kinachoelemea upande wa wakurd,HDP katika kongomano hili pia,ni ushahidi kwamba azma ya mshikamano ni ya kijuu juu. Ukweli ni kwamba Uturuki inasalia kuwa nchi iliyogawanyika. Kwa upande mmoja imedhihirika jinsi mamilioni ya wananchi walivyopania kuona wanajeshi hawanyakui madaraka na demokrasia inalindwa. Na kwa upande mwengine lakini Erdogan anatawala kwa kupitisha kanuni bila ya kutilia maanani demokrasia."

Hali ya kiuchumi ya marekani inanawiri

Ripoti yetu ya mwisho inamulika hali ya kiuchumi nchini Marekani. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika: "Obama alipoingia madarakani alirithi hali katika soko la ajira ambapo kila mwezi watu karibu laki nane walikuwa wakipoteza nafasi zao za kazi. Kwamba mwaka 2016 nafasi 186.000 za kazi zinabuniwa kila mwezi,hali hiyo inaashiria mabadiliko yaliyoweza kupatikana. Pekee mwezi uliopita wa Julai nafasi 255.000 za kazi zimeweza kupatikana. Asili mia 4.9 wamesajiliwa hawana kazi nchini Marekani, hicho kikiwa kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa muda mrefu sasa nchi humo. Kinachotia moyo zaidi upande wa serikali ni jinsi mishahara ilivyopanda na jinsi kiu cha wanunuzi kilivyoongezeka. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita,wanunuzi wamezidisha matumizi kwa asili mia 4.5 ikilinganishwa na miezi mitatu ya kabla ya hapo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga