Utayarishaji wa Katiba mpya ya Zimbabwe wakabiliwa na changamoto | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Utayarishaji wa Katiba mpya ya Zimbabwe wakabiliwa na changamoto

Baraza la vyama vya kiraia nalo laongoza mchakato mbadala wa kutengeneza katiba.

default

Rais Robert Mugabe (left), wa Zimbabwe akipeana mkono na Morgan Tsvangirai, Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Ikiwa ni wiki mbili sasa baada ya wafuasi wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuchelewesha hatua ya kutayarisha katiba mpya ya nchi hiyo, suala hilo linakabiliwa na changamoto nyingine, kufuatia baraza la vyama vya kiraia kuanzisha mchakato wa kutengeneza katiba mbadala, likisema kuwa bunge la serikali ya umoja wa kitaifa siyo la kidemokrasia na litatayarisha katiba yenye kasoro.

Baraza hilo linalojulikana kama NCA, linaongoza mchakato mbadala wa kutengeneza katiba ya nchi hiyo. Baraza hilo ni muungano wa mashirika ya wanawake, makanisa, vyama vya upinzani, vyama vya wafanyakazi na wanafunzi pamoja na vyama vya kiraia. Mwaka 1999, NCA ilifanya kazi na chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC), kuukataa muswada wa katiba ya serikali katika kura ya maoni.

Mwenyekiti wa NCA, Lovemore Madhuku, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa mchakato wa katiba unaofanywa na bunge pamoja na serikali usimamishwe haraka. Aidha, Madhuku ameongeza kuwa siyo kazi ya wanasiasa kuandika katiba na kwamba hawakuwachagua wabunge wao ili waandike katiba, bali walichaguliwa ili kuwahudumia wananchi. Mwenyekiti huyo wa NCA, anapendekeza kuwa mchakato huo wa katiba ufanywe na baraza huru litakalochaguliwa na wawakilishi wa wadau katika mkutano wa pamoja.

Katika mkutano uliofanyika Jumatatu ya wiki hii huko Chitungwiza nje kidogo ya Harare, wajumbe wa baraza hilo lilikubaliana kuanzia mwezi ujao wa Agosti, kuanza kutoa elimu kwa raia ya kuukataa mchakato wa katiba unaofanywa na wanasiasa. Kwa muda mrefu NCA imekuwa ikitaka kuwepo kwa katiba mpya ya kidemokrasia nchini Zimbabwe.

Farai Maguwu, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti na Maendeleo, anafuatilia kwa karibu michakato yote ya serikali vya vyama vya kiraia, ambapo amesema hatua hiyo ina manufaa kwa demokrasia ya Zimbabwe. Anasema kuwa serikali ina haki ya kuwa na mtazamo wake na haina mamlaka ya kuandika katiba kwa niaba ya wananchi, lakini wakati huo huo inatakiwa kupewa nafasi katika kuandaa mchakato huo.

Kamati ya katiba yenye wajumbe 25 inaongoza mchakato wa serikali, ambayo inaanza na mashauriano kwa miezi minne na baadaye muswada utatengenezwa. Muswada huo baadae utapelekwa katika mkutano wa pili wa wadau wote na kufuatiwa na mjadala wa mwezi mmoja bungeni. Uchaguzi wa kura ya maoni ya katiba mpya umepangwa kufanyika Julai mwaka 2010 na endapo itapitishwa, uchaguzi mpya wa wabunge, rais na serikali za mitaa nchini Zimbabwe utafanyika chini ya katiba mpya ya nchi hiyo.

Vyama vitatu vya siasa vya Zimbabwe vilisaini makubaliano ya kisiasa mwezi Septemba, mwaka 2008 ulioainisha mambo kadhaa ikiwemo kuundwa kwa serikali ya muungano baina ya chama tawala cha ZANU-PF, MDC na chama kingine kilichojitenga na MDC. kifungu cha 6 cha makubaliano hayo kinataka kuundwa kwa katiba inayozingatia matakwa ya wananchi.

Katiba ya sasa ya nchi hiyo imefanyiwa marekebisho mara 19 tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1980 na wakosoaji wanasema kuwa mabadiliko hayo yamesaidia tu kuuimarisha utawala wa Rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 29.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/IzkY
 • Tarehe 29.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/IzkY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com