1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Syria ulivunja makazi kuadhibu wapinzani

Josephat Nyiro Charo30 Januari 2014

Serikali ya Syria imeyaharibu kabisa maelfu ya makazi kama adhabu jumla dhidi ya jamii ambazo ziliuunga mkono upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus na katika mkoa wa Hama.

https://p.dw.com/p/1AzfT
Syrische Soldaten in Damaskus
Picha: picture-alliance/dpa

Katika ripoti yake iliyochapishwa hapo jana shirika la Human Rights Watch, limeishutumu serikali ya Syria kwa kuviangamiza kabisa vitongoji vizima kutoka kwenye ramani kwa kutumia matingatinga na vilipuzi. "Operesheni hii ya kuvunjavunja makazi ya watu ni tukio la hivi karibuni linaloongezea orodha ya uhalifu uliofanywa na serikali ya Syria," amesema Ole Solvang, mtafiti wa masuala ya dharura wa shirika hilo.

Shirika la Human Rights Watch limeorodhesha visa kadhaa vya uvunjaji mkubwa wa makazi kati ya mwezi Julai mwaka 2012 na Julai mwaka 2013, visa viwili vikifanyika katikati mwa mkoa wa Hama na vitano katika mji mkuu, Damascus na viunga vyake. Kwa kutumia picha za setilaiti, shirika hilo limesema lilikadiria eneo la jumla ya hekta 140, ikiwa ni sawa na viwanja karibu 200 vya mpira wa miguu, liliharibiwa kabisa. Limedokeza kwamba majengo mengi yaliyobomolewa yalikuwa na ghorofa kadhaa na maelfu ya watu walipoteza makazi yao.

Picha za kabla ya operesheni hiyo katika kitongoji cha Wadi al-Joz katika mkoa wa Hama zinaonyesha majengo kati ya barabara mbili kuu mwezi Aprili mwaka jana, lakini picha zilizochukuliwa baadaye zinaonyesha maeneo meupe sehemu ambazo awali majumba yalikuwa yamesimama mnamo mwezi Mei mwaka jana.

"Baada ya uvunjaji huo jeshi likikuja katika kitongoji chetu likisema kutumia vipaza sauti kwamba lingekiharibu kama lilivyoviangamiza vitongoji vya Wadi al-Joz na Masha al Arbeen, iwapo risasi moja tu ingefyetuliwa kutoka hapa," alisema mwanamke mmoja kutoka kitongoji jirani wakati alihojiwa na shirika la Human Rights Watch.

Ngome za upinzani zililengwa

Shirika hilo limesema maeneo yaliyoathirika yanaonekana kuwa ngome za upinzani na hakuna ushahidi kuunga mkono madai ya serikali kwamba operesheni hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za kupanga maeneo ya miji. "Harakati hizo zilisimamiwa na vikosi vya jeshi na mara kwa mara zilifuatiwa na mapigano katika maeneo hayo kati ya vikosi vya serikali na vya upinzani," limeongeza kusema shirika hilo.

Shirika la Human Rights Watch aidha limesema limefaulu kubaini kwamba hakujakuwa na operesheni kama hizo za kuyavunja makazi katika maeneo ambayo kwa ujumla yanaiunga mkono serikali. Wakaazi wameliambia shirika hilo kwamba walionywa kwa muda mfupi na hata wakati mwingine hawakuonywa kabisa kabla operesheni hizo kuanza na hawakulipwa fidia yoyote.

Anschlag auf Bushaltestelle in Damaskus, Syrien
Shambulizi katika mji wa DamascusPicha: REUTERS/SANA/Handout via Reuters

Mmiliki mmoja wa mgahawa katika kitongoji cha Qabun kaskazini mashariki mwa Damascus ameliambia shirika hilo kwamba alilazimishwa kuondoka eneo la uvunjaji wa makazi na kutishwa angetiwa mbaroni. "Kazi ya familia yangu iliharibiwa kwa sekunde moja mbele yangu nikiwa naangalia," aliliambia shirika hilo.

Mjini Damascus operesheni hiyo ilifanywa katika maeneo yanayoyazunguka maeneo yenye umuhimu kwa serikali, ukiwemo uwanja wa ndege.

Operesheni ni kinyume na sheria ya vita

Lakini shirika la Human Rights Watch limesema uharibifu huo ulikiuka sheria ya vita kwa sababu haukuwa na maana yoyote kijeshi na unaonekana ulinuia kuwaadhibu raia au kwa kuwa ulisababisha machungu yasiyo na mithili kwa raia. Ripoti hiyo imesema "wale wote waliohusika na uharibifu huo wa mali ya umma au kuweka adhabu jumla wamefanya uhalifu wa kivita na wanapaswa wachunguzwe na kuwajibishwa."

Ole Solvang, mtafiti wa shirika la Human Rights Watch amesema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitia agizo la mahakama ya kimatafa ya uhalifu, ICC, linatakiwa kutuma ujumbe wa wazi kwamba kuufunika ukweli na uhalifu unaofanywa na serikali bila hofu ya kuadhibiwa hautakwamisha kupatikana haki kwa wahanga.

Der syrische Präsident Bashar al-Assad während eines Interviews für AFP
Rais wa Syria, Bashar al AssadPicha: AFP/Getty Images

Katika taarifa yake upinzani wa Syria umesema kuwatesa raia ili waachane na miito ya kutaka uhuru ni mkakati wa serikali. Umerudia mwito wa kumtaka rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, ang'atuke na utawala wake ukabiliwe na mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague, Uholanzi.

Zaidi ya watu 130,000 wameuwawa tangu kuanza mzozo wa Syria Machi 2011, huku mamilioni wengine wakilazimika kuwa wakimbizi nchini mwao au kuvuka mipaka na kuwa wakimbizi katika nchi jirani.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman