1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Utandawazi uwe na usawa"

Peter Stützle / Maja Dreyer1 Februari 2007

Sera nzuri za kuleta maendeleo katika nchi maskini zinazinufaisha pia nchi zilizoendelea. Haya aliyasema Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alipohutubia mkutano maalum kuhusu sera za maendeleo wa chama chake cha Christian Demokratik Union CDU.

https://p.dw.com/p/CHKx
Utandawazi unamnufanisha nani?
Utandawazi unamnufanisha nani?Picha: DPA

Ujerumani inafaa kuhakikisha utandawazi unakwenda sawa. Pamoja na hayo Angela Merkel alitaja matumaini yake mazuri kuwa mazungumzo ya Doha juu ya kulegeza soko la biashara duniani.

Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya maendeleo katika nchi maskini, Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul, ni wa chama cha Social Demokrats, SPD, ambacho kawaida kinajihusisha zaidi na masuala haya.

Lakini pia vyama ndugu vya kihafidhina, CDU/CSU, ambacho kiko pia katika serikali hii ya mseto, vilitaka kuonyesha kuwa vinajali jambo hilo. Kansela Merkel alitumia nafasi ya kongamano hili lililofanyika jana usiku kutoa hotuba juu ya msingi wa sera zake za maendeleo. Bi Merkel alisisitiza hasa fursa nzuri ya utandawazi kutokana na biashara na kubadilishana teknolojia kati ya nchi tajiri na nchi maskini. Alisema: “Lakini licha ya fursa hizo kuwepo, tunaona kuwa kuna mipasuko mikubwa duniani ambayo hata inazidi kukuwa kuliko kupungua, na kuna mifano mibaya katika nchi nyingi.”

Kinachohitajika ni kuleta usawa katika utandawazi. Merkel alikumbusha msingi wa sera za maendeleo ambao ni wa maadili. Sababu Ujerumani inajihusisha na maendeleo katika nchi nyingine ni kusaidia binadamu. Upendo kwa jirani yako na kuheshima hadhi ya mwanadamu ni muhimu sana katika sera hizo, alisema Angela Merkel. Lakini sera hizo pia ni kwa manufaa ya Ujerumani: “Sera nzuri za maendeleo zitazinufaisha nchi za kiviwanda sawa na nchi zinazoendelea, kwa vile masuala ya nishati, upatikanaji rasilimali, usalama na amani yanatuhusu sisi sote na mustakabali wa sisi sote.”

Kansela huyu alitaja pia matumaini mazuri kwamba mazungumzo ya Doha kuhusu kulegeza biashara ya dunia yataendelea, lakini wakati huo huo akataka kuweko maelewano kuwa Umoja wa Ulaya unasisitiza kuwepo masharti fulani, kama vile kuwepo viwango vya chini katika utengenezaji wa bidhaa.

Bi Merkel alitaja pia kuhusu mjadala unaofanyika nchini Ujerumani ikiwa nchi kama China ambazo zinakuwa haraka kiuchumi bado zinafaa kupewa msaada wa maendeleo. Kansela Merkel alisema msaada unapaswa kutolewa katika sekta fulani, mfano katika ulinzi wa hali ya hewa kwa kutumia teknolojia za kisasa ambazo zinapunguza matumizi ya nishati. Kwa upande mwingine lakini Bibi Merkel alidai kuwa: “Pale ambapo mafundi ya kompyuta – na sana nazungumzia India – wanafanya kazi vizuri au hata kuliko mafundi wa Ulaya, basi nchi hizo zichukue hatua ili kuwasaidia mamillioni ya wakulima maskini kuwa na maisha bora.

Askofu wa Accra, Ghana, ambaye pia alihudhuria kongamano hilo la vyama vya kihafidhina vya Ujerumani aliwataka wananchi wa Ulaya kutoweka utamaduni wao kama msingi wa maendeleo. Askofu huyu alisema kuwa Afrika inapaswa kuwa na maadili yake ya kienyeji.