1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utajiri wa binti wa rais wa Angola

25 Oktoba 2016

Isabel Dos Santos ni binti wa kwanza wa Rais Jose Eduardo Dos Santos wa Angola na anamiliki utajiri wa kiasi dola bilioni 3.2 za Kimarekani, unaomfanya kuwa ndiye mwanamke tajiri kabisa barani Afrika.

https://p.dw.com/p/2Rgpv
Angola Isabel dos Santos spricht zu Journalisten
Angola Isabel dos Santos binti wa kwanza wa rais wa Angola mwenye utajiri mkubwa barani AfrikaPicha: Reuters/E. Cropley

Binti huyo amejijengea himaya yake kwa mapana na marefu na hasa katika mji mkuu Luanda ambao ni miongoni mwa miji ya kifakhari na ghali kabisa duniani.Unapotembea katika mji mkuu wa Angola, Luanda, ni vigumu sana kushindwa kuitambua au kukumbana na alau kampuni moja ya Isabel Dos Santos. Binti huyo wa kwanza wa Rais Eduardo Dos Santos na ambaye ni mwanamke tajiri kabisa barani humo amejenga himaya yake ya utajiri katika moja ya miji ghali kabisa duniani -kutoka sekta ya mawasiliano, benki, televisheni ya setelaiti hadi kwenye spoti - kote huko anamiliki biashara kubwa zenye majina mjini Luanda.

Isabel anahodhi kampuni ya Unitel, ambayo ni kampuni kubwa kabisa ya simu za mkononi nchini Angola ikiwa na matawi 81 ndani ya mji huo mkuu pekee na zaidi ya wateja milioni 10 nchi nzima. Anamiliki msururu wa maduka makubwa, huku akiwa pia na hisa katika mabenki ya BIC na BFA sambamba na katika kampuni ya saruji ya Nova Cimangola.

Umiliki wa kampuni kubwa za mafuta

Afrika Angola Candango Supermarkt in Luanda
Moja kati ya maduka makubwa yanayomilikiwa na Isabel dos SantosPicha: DW/P. Borralho

Na kama haitoshi, mwanamama huyo anasimamia kampuni kubwa ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Sonangol pamoja na klabu ya soka ya Petro de Luanda inayofadhiliwa na kampuni yake.

Almuradi, orodha ya utajiri wa Isabel Dos Santos ni ndefu ikijumuisha pia sekta ya afya na uhusiano wake na kliniki kubwa kubwa nchini humo bila ya kuiweka kando sekta ya biashara ya madini, anasema mwanachama wa upinzani, Nelito Ekuikui:
''Tunaweza kuzungumzia pia sekta ya afya na uhusiano wake na kliniki kubwa kubwa za humu nchini bila ya kusahau sekta ya madini. Kampuni hiyo  hazina ushindani. Hilo ni tatizo kubwa kwa nchi kwa sababu ni vigumu sana kwa wafanyabiashara wengine. Endapo tungekuwa na wafanyabiashara  wapya tungekuwa na nafasi nyingi za ajira.''

Taswira ya Isabel kwa Waafrika

Baadhi ya watu wanamuangalia Isabel Dos Santos kama mfano wa wafanyabiashara barani Afrika ambao wametoa nafasi za ajira zinazohitajika kwa kiasi kikubwa, katika taifa ambalo asilimia 24 ya watu hawana kazi, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014. Lakini Nelito Ekuikui haliangalii suala hilo kwa jicho sawa na hilo. Yeye anasema utajiri wa Isabel na biashara zake nchini Angola hazina mpinzani na hilo ni tatizo. Mwanaharakati wa Angola, Benmedoto Jeremias, anasema kwamba kuwa binti wa rais wa nchi kumemrahisishia mwanamama huyo shughuli zake zote ikilinganishwa na wawekezaji wengine, ''Kila kitu anachokimiliki Isabel Dos Santos kimetokana na upendeleo na fursa anazopata kutoka kwa baba yake. Sio mali alizopata kwa juhudi zake''

Kwa upande mwingine, mwandishi habari Rafael Marques ambaye amekuwa akifuatilia mzizi wa utajiri wa Isabel Dos Santos kwa kipindi cha miaka mingi, anasema kwamba baba yake, Jose Eduardo Dos Santos, amekuwa na dhima kubwa katika kumjengea utajiri huo.

Mwandishi huyo wa habari wa Angola aliiambia DW mapema mwaka huu kwamba kila alichokitaka Isabel, baba yake alihakikisha anakipata. Dos Santos alitumia hadi nafasi yake kama rais kumpa mwanamwe huyo majukumu ya kusimamia fedha katika mikataba mikubwa mikubwa ya serikali, ingawa mara nyingi Isabel amekuwa akizipinga tuhuma hizo za kupendelewa.

Na baada ya kuiongoza kampuni kubwa ya nishati ya mafuta ya Sonangol na kufikia hatua hadi ya kuwa mwekezaji mkubwa nchini Ureno, mkoloni wa zamani wa Angola, wapinzani wanahisi hana tena pa kwenda na sasa huenda akageukia kujaribu katika siasa. Mwanaharakati Benedito Jeremias anakubaliana na hilo akisema mrembo huyo wa miaka 43 huenda ikawa hata ana mipango ya kukirithi kiti kinachokaliwa na baba yake.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/Guilherme Correia da Silva

Source: DW-English Page

Mhariri: Mohammed Khelef