1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Mashariki

9 Mei 2009

Ushirikiano mpya wa Umoja wa Ulaya na nchi sita ambazo hapo zamani zilikuwa jamhuri za iliyokuwa Soviet Union, umesababisha wasiwasi nchini Urusi.Lakini, hali hiyo inaweza kubadilishwa.

https://p.dw.com/p/Hm06
EU-Gipfeltreffen zur Östlichen Partnerschaft in Prag
Mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Mashariki mjini Prague.Picha: picture-alliance/ dpa

Ushirikiano huo mpya ni wa nini? Kwani hivi sasa Umoja wa Ulaya una mengi ya kushughulikia kwa sababu mkataba wake wa mageuzi bado haujapatiwa ufumbuzi. Wakosoaji wengi wanaonya dhidi ya kupokewa kwa wanachama zaidi. Lakini ushirikiano na nchi hizo za Ulaya ya Mashariki hauhusiki na uanachama.Wala si hatua ya kwanza kwa nchi hizo kuingia katika Umoja wa Ulaya.

Mwaka jana,Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kwa mbwembwe na shamrashamra alianzisha umoja wa nchi za Bahari ya Mediterania ambazo hupakana na Umoja wa Ulaya upande wa kusini. Hoja yake ni kuwa matatizo ya majirani hao vile vile ni matatizo ya Umoja wa Ulaya. Matatizo hayo yanasababishwa na hamu ya kukimbilia Ulaya, miundo ya kitaifa iliyo dhaifu, pamoja na migogoro ya nchi au matatizo ya mazingira. Hayo yote yanakubalika.

Lakini Sarkozy hakuhudhuria mkutano wa Prague uliohusika na ushirikiano mpya. Hata viongozi wa nchi na serikali za Uingereza,Italia na Uhispania walibakia nyumbani. Hoja za Sarkozy kuhusu umoja wa Bahari ya Mediterania ni halali pia kwa Ushirikiano wa Mashariki. Ni maslahi ya Umoja wa Ulaya pia kutaka kuona majirani wa mashariki wakifanya maendeleo ya kidemokrasia na kiuchumi na wakitenzua migogoro yao.

Kwa kweli tatizo ni Urusi iliyoueleza ushirikiano huo mpya kama ni jeribio la kueneza ushawishi wa Umoja wa Ulaya hadi katika mipaka yake. Mara nyingine tena Urusi ina hofu kuwa inajongelewa na Umoja wa Ulaya sawa na hofu zake kuhusu kupanuliwa kwa Shirika la Kujihami la Magharibi NATO.Lawama hizo ni upuuzi mtupu.Tofauti kubwa iliyokuwepo kati ya Moscow na Brussels ni kwamba Urussi inataka kueneza ushawishi wake kwa mabavu na Umoja wa Ulaya unatoa mapendekezo ya kuvutia ukiwepo uhuru wa kukubali au kukataa -hakuna anaeshurutishwa. Je, ni kosa la Umoja wa Ulaya kuwa nchi hizo za ushirikiano zinageukia kambi ya Magharibi?

Kwa upande mwingine lakini ni sera za Urusi za kujitapa kuhusu nishati yake, ndio zilizosababisha Umoja wa Ulaya kutupia jicho kwengineko.Hata hivyo, mtu anapswa kuwa muangalifu,pale Urusi inapohusika kwani nchi hiyo ina sauti na itaendelea kuwa na usemi, hasa katika sekta ya kijeshi na nishati.Lakini hiyo haimaanishi kwenda umbali wa kuachana na ushirikiano wa mashariki. Kwa hivyo,lengo la Umoja wa Ulaya liwe hili: kuisadikisha Urusi kuwa hata nchi hiyo itanufaika ikiwa utulivu wa kiuchumi na kisiasa utapatikana katika eneo hilo yaani kila mmoja atanufaika kutokana na Ushirikiano huo wa Mashariki.

Mwandishi: C.Hasselbach

Mhariri: Othman Miraji