1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ni tishio kwa amani - PLO

Mohammed Khelef18 Machi 2015

Ushindi wa Benjamin Netanyahu wa Israel umepokelewa kwa tahadhari na jamii ya kimataifa na Wapalestina, hasa kutokana na utata wa mchakato wa amani unaoambatanishwa na uundwaji wa taifa huru la Palestina.

https://p.dw.com/p/1Eskm
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Reuters/N. Elias

Kama ilivyotazamiwa, wanasiasa wa ngazi za juu wa chama cha Republican nchini Marekani wamemtumia Netanyahu salamu za pongezi, wakiuita ushindi wake kuwa ulimstahikia. Jeb Bush, kaka wa rais wa zamani George Bush na pia mtu anayetarajiwa kugombea urais wa Marekani mwakani kwa tiketi ya Republican amemsifu Netanyahu kuwa ni kiongozi wa kweli ambaye ataendelea kuiweka Israel salama na imara.

Salamu kama hizo zimetoka pia kwa chama chengine cha kihafidhina cha Tea Party, ambapo seneta Ted Cruz ametumia nafasi hiyo kumkosoa Rais Barack Obama kwa kuwa na mahusiano mabaya na Netanyahu.

Hata hivyo, Iran imeupuuza ushindi huo wa Netanyahu ikisema hauna umuhimu wowote si kwa Wapalestina wala kwa ulimwengu wa Kiislamu, kwani vyama vyote vya kisiasa nchini Israel viko sawa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Marzieh Afkham, amesema vyama vyote vina tabia moja ya uchokozi na mateso dhidi ya Wapalestina na kupanga hujuma dhidi ya mataifa ya Kiislamu.

Abbas asisitiza suluhisho la mataifa mawili

Kwa upande wake, Rais Mahmoud Abbas wa Palestina alisema kimsingi serikali yake haijali nani anachukuwa uongozi wa taifa la Israel, bali inachojali hasa ni kile anachokisimamia kiongozi huyo kwenye suala tete la mzozo kati ya Palestina na Israel.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina.
Rais Mahmoud Abbas wa Palestina.Picha: picture-alliance/dpa/Alaa Badarneh

Msemaji wa Abbas, Nabil Abu Rudeineh, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba "Palestina itafanya kazi na serikali yoyote ya Israel ambayo inakubaliana na suluhisho la mataifa mawili huru."

Hata hivyo, ni upinzani kwa suluhisho hilo ndio ambao wengi wanadhani kwamba ulimpatia ushindi Netanyahu kwenye uchaguzi huo wa jana, baada ya mwenyewe Netanyahu kuigeuka imani yake ya muda mrefu ya kuwapo kwa mataifa mawili yanayoheshimiana katika dakika za majeruhi, kuwavutia wapiga kura wenye msimamo mkali wa Kizayuni.

PLO yamkosoa Netanyahu

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, Hannan Ashrawi, amesema kuchaguliwa tena kwa Netanyahu kumetokana na sera zake za kupandikiza khofu, uadui na hali ya kukosa kujiamini ndani ya jamii ya Israel.

"Kwa kuharibu fursa ya amani, kuwakatalia Wapalestina haki ya kuwa na taifa, kuvuruga kwa makusudi sheria za kimataifa na kupingana na dhamira ya jamii ya kimataifa kwa kuendeleza ujenzi wa makaazi ya walowezi na wizi wa ardhi, Netanyahu ni mzigo na ana dhamana kwenye kuliingiza eneo hili kwenye siasa kali na machafuko zaidi," alisema Ashrawi.

Umoja wa Ulaya ulimpongeza Netanyahu kwa ushindi huo, ukisema bado una dhamira ya kushirikiana na serikali mpya ya Israel kuufufua mchakato wa mazungumzo ya amani na Wapalestina. Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo, Federica Mogherini, alisema "amani ya Mashariki ya Kati ina umuhimu mkubwa pia kwa Ulaya."

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters,dpa,AFP
Mhariri: Josephat Charo