1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushawishi wa OPEC kuhusu bei ya mafuta duniani

P.Martin13 Mei 2008

Nchi wanachama wa OPEC-shirika la nchi zinazozalisha mafuta,huchangia asilimia 40 ya mafuta ulimwenguni na humiliki zaidi ya robo ya akiba ya mafuta kote duniani.

https://p.dw.com/p/DzGh

Baada ya mataifa mengine yasio wanachama wa OPEC kuvuka kiwango chao cha uzalishaji wa mafuta,ni dhahiri kuwa ushawishi wa OPEC utazidi kuwa na nguvu huku bei ya petroli ikizidi kuongezeka.

Kawaida mawaziri wa mafuta wa nchi wanachama 13 wa OPEC hukutana mwaka mara mbili katika mji mkuu wa Austria, Vienna.Ingawa si nchi zote zinazozalisha mafuta ni wanachama,shirika la OPEC lina usemi mkubwa na litaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika utaratibu wa kupanga bei ya mafuta.Hivi sasa wito ni huu:Uzalishaji wa mafuta hautopigwa jeki-kwa hivyo mafuta yataendelea kuwa ghali.Lakini Waziri wa Mafuta wa Algeria Chakib Kheli alie Rais wa OPEC anasema:

"Kwa kweli uamuzi uliopitishwa ni wa busara.Kuna mafuta ya kutosha katika masoko.Kama ilivyokuwa hiyo miaka mitano iliyopita,tunategemea kuona mahitaji yakipunguka."

Robo tatu ya akiba ya mafuta iliyopo duniani,hukutikana katika majangwa ya nchi za OPEC.Hata hivyo,haimaanishi kuwa mataifa hayo daima hukubaliana katika masuala yote.Kwani kisiasa wanachama hao wanatofautiana. Baadhi yao,kama vile Saudi Arabia,wanataka uhusiano mzuri pamoja na nchi za Magharibi.Wengine hutumia bei ya mafuta kama silaha ya kisiasa kupambana na mataifa ya Magharibi.Mfano mmoja ni Iran.

Lakini licha ya tofauti hizo,biashara na fedha ni mambo yanayowafungamanisha wanachama hao wa OPEC hasa yanapozuka masuala ya kupanga kiwango cha mafuta yatakayozalishwa na hivyo kushawishi bei ya mafuta.

Hivi sasa,bei ya mafuta inaendelea kuongezeka na kila mwezi huvunja rekodi.Kiasi ya miaka kumi iliyopita,pipa moja la mafuta liligharimu kama Dola 10-na mwaka huu kwa mara ya kwanza bei imevuka kiwango cha Dola 100 na wala hakuna anaejua itaishia wapi.

Wengi huuliza nini husababisha mkondo huo.Kuna sababu nyingi.Lakini sababu mojawapo kuu na mahitaji ya mafuta yanayozidi kuongezeka kila siku.Kwani maendeleo ya kiuchumi hutegemea mafuta na hivi sasa,katika nchi nyingi barani Asia kama vile India na China kuna mfumko wa kiuchumi.Mahitaji ya mafuta katika nchi hizo yanazidi kuongezeka kila kukicha.

Sababu nyingine ya kuongezeka kwa bei ya mafuta ni kwamba kwa sehemu kubwa mafuta hupatikana katika maeneo ya migogoro kama vile Mashariki ya Kati.Na hata vita na mashambulizi ya kigaidi yanayolenga mabomba ya mafuta kama huko Nigeria,hupunguza uzalishaji wa mafuta.Na matukio kama hayo huathiri masoko ya mafuta moja kwa moja na mara bei huongezeka.Hata hivyo bei ya mafuta haiongezeki panapofanywa mashambulizi tu.Hata kitisho cha uwezekano wa kuzuka mapambano ya kijeshi,kwa mfano Marekani kuivamia Iran,basi hutosha kupandisha bei ya mafuta.Katika hali kama hiyo ni shida kutaraji kuwa bei ya mafuta huenda ikapunguka katika siku hizi zijazo.