Usalama waimarishwa Libya
17 Februari 2013Mipaka imefungwa na baadhi ya safari za ndege za kimataifa zimefutwa kwa muda huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa ghasia mpya.
Maadhimisho hayo ya vuguvugu la mapinduzi ambalo lilimalizika kwa kuuwawa kwa Gaddafi hapo Oktoba 2011 yanakuja wakati viongozi wapya wa Libya wanakabiliana na wakosoaji ambao wanatoa wito wa kile kilichoelezwa kuwa ni "mapinduzi mapya", na wanawashutumu viongozi hao kwa kushindwa kuleta mageuzi ambayo yanahitajika sana.
Siku ya Ijumaa , maelfu ya watu walikusanyika katika miji mkuu ya Tripoli na Benghazi kusherehekea mwanzo wa maandamano hayo Februari 15, 2011, ambayo yalizusha uasi siku mbili baadaye.
Hakuna sherehe rasmi
Hakuna mpango maalum rasmi ulioandaliwa na serikali kwa ajili ya maadhimisho haya leo Jumapili(17.02.2013), lakini maafisa wamechukua hatua zenye lengo la kuzuwia ghasia zozote katika siku hii ambayo sherehe za bila kupangwa zinatarajiwa.
Mipaka ya Libya na Misri na Tunisia imefungwa kuanzia Alhamis kwa muda wa siku nne, na safari zote za ndege za kimataifa zimefutwa kwa muda, isipokuwa katika uwanja wa ndege wa Tripoli, na mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Benghazi, ambao ulikuwa ni shina la uasi wa hapo Februari 17.
Waziri mkuu Ali Zeidan amesema kuwa hatua hizo zilichukuliwa ili kuepuka , "juhudi zozote za kuchafua usalama wa Libya na kuharibu sherehe za maadhimisho hayo ya mapinduzi.
Vizuwizi vya barabarani pia vimewekwa katika mji mkuu Tripoli na Benghazi.
Wito wa kukaidi sheria
Makundi ya upinzani yanadai kuwa maafisa wa zamani wa utawala wa Gaddafi wanazuiwa kushika nyadhifa za umma, na vijikaratasi vilivyosambazwa mjini Tripoli vinatoa wito wa " kufanyika uasi wa umma", na umma kutofuata sheria ili kuiangusha serikali ya hivi sasa.
Haijafahamika wazi ni nani anahusika na vijikaratasi hivyo na wito huo wa kufanya upinzani, lakini maafisa wa Libya pamoja na mashirika kadha , ikiwa ni pamoja na makundi ya Kiislamu, wanashutumu mabaki ya utawala wa zamani kwa kuchochea ghasia , ili "kupandikiza hali ya kutokuwa na amani na vurugu".
Maafisa wamesema kuwa vibali maalum vitahitajika kwa ajili ya kufanyika "maandamano ya amani", na wametishia kutumia nguvu dhidi ya mtu yeyote atakayejaribu kuchafua maadhimisho hayo.
Benghazi waanzisha vikundi vya kujilinda
Wakaazi wa mji wa benghazi , ambao wameathirika na ghasia zinazohusishwa na makundi ya Waislamu wenye itikadi kali ambao wanaelekeza ghasia zao dhidi ya mashirika ya kimataifa pamoja na balozi mbali mbali , wameweka vikundi vya ulinzi katika maeneo yao.
Mji huo ulikumbwa na ghasia tarehe 11 mwezi Septemba mwaka jana kutokana na shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani ambapo balozi wa Marekani Chris Stevens aliuwawa pamoja na watu wengine watatu raia wa Marekani.
"Suala la usalama ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo, hususan kuenea kwa silaha na maelfu ya wafungwa kukimbia kutoka jela , wakati wa mapinduzi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Suleyman Azqim ameliambia shirika la habari la AFP.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Stumai George