1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa ndani bado mada tete magazetini

Admin.WagnerD27 Desemba 2010

Masuala matatu ndiyo leo (27 Disemba 2010) yaliyozungumzwa na magazeti ya Ujerumani: urasmishaji wa shughuli za wajasiriamali, mgongano baina ya siasa za ndani na usalama na walakini kwenye ndoa ya vyama vya CDU na FDP.

https://p.dw.com/p/zqEV
Otto Kentzler, Rais wa Shirikisho la Kazi za Mikono la Ujerumani
Otto Kentzler, Rais wa Shirikisho la Kazi za Mikono la UjerumaniPicha: ZdH

Rais wa Shirikisho la Kazi za Mikono la Ujerumani, Otto Kentzler, sasa anasema kwamba ni lazima kwa vijana wajasiriamali kupatiwa vyeti maalum vinavyotambua ujuzi na uwezo wao, maana kwa hakika wanafanya mambo mengi makubwa kama au hata kuliko wale waliokwenda vyuoni kusomea taaluma hizo hizo.

Gazeti la Saarbrücker Zeitung linaunukuu mwito wa Mhandisi Kentzler, kwamba una maana kubwa kwa mustakabali wa wajasiriamali.

"Tunatambua pia kwamba, vijana wetu wengi wanataka elimu na ujuzi, ambao wanaweza kuuthibitisha kwenye soko la ajira", ndivyo anavyosema Kentzler.

Na mwaka 2011 una kila fursa ya kuona kwamba hayo yanafanyika kwa kuwapa vijana hawa utambulisho, maana kwa hakika wamejituma vya kutosha kuweza kufika walipofika. Haikuwa kazi rahisi kujifunza na kuumudu ujuzi walionao, na hivyo ni stahiki yao kutambuliwa, maana kama asemavyo Kentzler "nao pia wana matarajio ya kuitwa vijana waliofuzu kwa viwango na sifa."

Mwaka wa 2010 ndio unamalizika hivyo, na katika mambo ambayo yaligonga vichwa vya wanasiasa na pia vya wanahabari, ni lile la usalama wa ndani. Na sasa yaonesha mwaka mpya wa 2011 unaingia ni kizigo kile kile cha mwaka unaomalizika, kwa mgongano baina ya wanasiasa na wanausalama linapokuja suala la usalama wa raia na maisha yao.

Kama linavyoandika gazeti la Mitteldeutsche Zeitung, kiongozi wa mseto wa CDU/CSU kwenye Bunge la Shirikisho, Hans-Peter Uhl, amemuonya mkuu wa Idara ya Kupambana na Uhalifu ya Ujerumani, Jörg Ziercke, dhidi ya upinzani wake kwa mipango ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Thomas de Maiziere, ya kulichanganya jeshi la polisi.

Uhl amefika umbali wa kumtisha Ziercke kwamba akae akijua kuwa idara yake iko chini ya de Maiziere akiwa kama waziri, na kama anapingana na maamuzi ya mkubwa wake ofisini, ajitayarishe na matokeo.

Na gazeti la Rheinische Post linakuja na utabiri wa kuvunjika kwa ndoa ya wapenzi wawili wasioaminiana, vyama vya CDU na FDP, ingawa Katibu Mkuu wa CDU, Hermann Gröhe, anasema kwamba kila usuhuba ukiimarika, ndipo uwezekano wa kufikia muafaka unapozidi kuongezeka baina ya vyama vyao.

Ni jambo jema sana, munapokuwa kwenye mseto kama huu, mukawa munafahamiana kwa kila jambo, kama asemavyo Gröhe, lakini hilo si jambo linalotokea kila mara. Kuna wakati ubia wenu huingia dosari, kwa ama yale yaliyopo baina yenu au kwa yale aliyonayo mmoja wenu.

Kwa mfano, hivi sasa mgogoro unaorindima chini kwa chini kwenye FDP, ambapo mmoja wa viongozi wa chama hicho, Guido Westerwelle, anaandamwa na wenzake. Kwa Gröhe anaona kuwa si jambo la haki hata kidogo kwa FDP kumtupia kila lawama Westerwelle peke yake. Bila ya shaka akihofia kuwa kinachotokea ndani ya FDP huenda kikaiua ndoa na CDU.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA

Mhariri: Josephat Charo