1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama kuimarishwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa

P.Martin6 Februari 2008

Umoja wa Mataifa ulioeleza wasi wasi wake kuhusu usalama wa wafanya kazi wake nchini Algeria na Sudan,sasa unakabiliwa upya na tatizo hilo katika maeneo mengine mawili:- Chad na Kenya.

https://p.dw.com/p/D3Bj
Secretary-General of the United Nations Ban Ki-moon speaks during a media conference at the World Economic Forum in Davos, Switzerland, Friday Jan. 25, 2008. Buoyed by a burst of optimism from Bill Gates, business and government leaders attending the World Economic Forum were set Friday to hear more about positive things they can do after two days of confronting fears. (AP Photo/Peter Dejong)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-MoonPicha: AP

Kufuatia machafuko ya nchini Chad na Kenya,Umoja wa Mataifa mara nyingine tena unachunguza usalama wa wafanyakazi wake katika nchi hizo mbili,ikiwa ni kama majuma manane tu tangu kupoteza wafanya kazi 11 katika shambulizi la bomu lililofanywa nchini Algeria kati kati ya mwezi Desemba.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipozungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne alisema,ameingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama katika mji mkuu wa Chad,Ndjamena.Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wameondoshwa Chad na wamepelekwa nchi za jirani-Kamerun na Gabon kwa msaada wa serikali ya Ufaransa,kwa sababu usalama wa watumishi hao hauwezi kuhakikishwa.Waliobakishwa ni wale wenye kazi muhimu za dharura.Lakini hao pia watahamishwa ikiwa hali ya kisiasa na kijeshi itadhoofika zaidi nchini humo.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon vile vile ameeleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa ofisi za Umoja wa Mataifa na watumishi wake kufuatia machafuko yanayotapakaa katika baadhi ya nchi za Kiafrika.Amesema matukio ya hivi karibuni nchini Kenya,Chad,Algeria na Darfur-magharibi mwa Sudan yanasisitiza hatari zinazowakabili watumishi hao.Ban anatazamia kuzungumza na wanachama 192 wa Umoja wa Mataifa na kuhimiza kuimarisha usalama wa watumishi wa umoja huo katika nchi zao.

Kwa mujibu wa Kemal Dervis,mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na miradi ya Maendeleo UNDP, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika takriban nchi sita,wameshauriwa kufanya kazi majumbani mwao kwa sababu baadhi ya ofisi zao zinalengwa na makundi ya kigaidi.Isipokuwa kwa Algeria afisa huyo alikataa kuzitaja nchi zingine.

Ban vile vile ametangaza kuundwa kwa jopo huru kushughulikia usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kote duniani.Jopo hilo litaongozwa na aliekuwa waziri wa nje wa Algeria,Lakhdar Brahimi.Mualgeria huyo vile vile aliwahi kuwa mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afghanistan,Haiti na Irak.

Alipozungumza juu ya Kenya,Ban alisema kuwa juma lililopita aliouonya mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika juu ya hatari ya kutapakaa kwa machafuko ya kikabila.Na kuhusu Chad alitoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukomesha mzozo huo.Upande wa Darfur alisema ukosefu wa usalama ni tatizo linaloendelea kukwamisha huduma za misaada kwa raia wanaohitaji misaada ya dharura.Akaongezea kuwa zile nchi zilizotoa mwito wa kuingilia Darfur zina wajibu maalum kutimiza ahadi zilizotolewa.Pendekezo la kupeleka vikosi vya kimataifa vya wanajeshi 26,000 kulinda amani Darfur halijatekelezwa kwa sababu ya uhaba wa vikosi na zana za kijeshi.

Isitoshe,serikali ya Sudan pia inapinga kuruhusu vikosi kutoka Thailand,Nepal,Norway na Sweden ikishikilia vikosi vya amani vitoke nchi za Kiafrika tu.Hadi hivi sasa ni wanajeshi 9,000 tu waliopatikana kutoka jumla ya 26,000 iliyopendekezwa.