1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usain Bolt awapagawisha mashabiki

Admin.WagnerD15 Agosti 2016

Usain Bolt akaribia kunyakua medali tatu nyingine za dhahabu katika olimpiki , mashabiki wake wapagawa mjini Rio. Katika siku ya 12 ya michezo ya Olimpiki, medali 17 zatafuta wenyewe Jumatatu(15.08.2016):

https://p.dw.com/p/1Jif2
Brasilien Olympische Spiele in Rio Sprinter Usain Bolt
Usain Bolt akikata mbuga akiwaacha wapinzani wake nyumaPicha: Getty Images/C. Spencer

Usain Bolt aliwashinda wapinzani wake na kunyakua medali ya tatu mfululizo katika michezo ya Olimpiki katika mbio za mita 100 na kujitangaza kwamba ana imani ya kuwa mtu asiyeshindika wakati mashindano haya ya mjini Rio yatakapofikia tamati.

Brasilien Olympische Spiele in Rio - Sprinter Usain Bolt
Usain Bolt akishangiria medali ya dhahabu katika mbio za mita 100Picha: Getty Images/C. Spencer

Akitaka kufuata nyayo za Wayde van Niekerk wa Afrika kusini aliyeweka rekodi ya dunia katika mbio za mita 400 , Mjamaica huyo alichomota na kumpita mpinzani wake kutoka Marekani Justin Gatlin na kunyakua tuzo hiyo ya juu kabisa ya Olimpiki kwa sekunde 9.81.

Akiwa na taji la kwanza kibindoni , Bolt alishangiria na kisha kusema anaelekeza fikira zake katika kuwania medali za dhahabu katika mbio za mita 200 na 100 mara 4 katika mashindano ya olimpiki kwa mara ya tatu mfululizo.

Mashabiki wake waliojazana mjini Rio jana walikuwa katika hali ya furaha tele kumuona bingwa wao akifanya kile walichotarajia.

Rio Momente 14 08 Leichtathletik 100 m Männer Finale Usain Bolt
Usain Bolt akionesha sekunde alizotuimia kushindaPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Mungu wangu !!! Bingwa aliyehai amethibitisha kwa mara nyingine tena, najisikia fahari kubwa kuwa Mjamaica."

"Furaha kupita kiasi, Nimefarijika sana ! Usain Bolt kwa dunia ! "

"Maneno hayawezi kuelezea , Nimefarijika sana , nimefurahi na nina raha sana, Usain Bolt ni mmoja kati ya wanariadha mahiri sana."

"Najisikia vizuri sana ! Usain Bolt kwa dunia ! Mara ya tatu na ya mwisho ambayo angefanikiwa , na amefanikiwa, nafasi ya kwanza duniani ! Olimpiki tatu mfululizo ! Usain Bolt !!

Commonwealth Games David Lekuta Rudisha
David Lekuta Rudisha wa KenyaPicha: AP

Washindi wengine wa medali za dhahabu katika fainali 22 za michezo ya olimpiki mjini Rio jana Jumapili ni pamoja na Jemima Sumgong wa Kenya katika mbio ndefu za Marathon , kuruka umbali mara tatu , Triple jump , Caterine Ibarguen wa Colombia , na Wayde van Niekerk wa Afrika kusini katika mbio za mita 400 pamoja na mpiganaji ndondi katika uzito mwepesi wa mdudu light - Flyweight Hassanboy Dusmatov wa Uzbekistan alijinyakulia pia medali ya dhahabu.

Mbio mita 800

Leo Jumatatu kuna medali 17 za dhahabu zinazotafuta wenyewe , ambapo michezo ya uwanjani na mbio zitashuhudia fainali tano ambapo David Rudisha kutoka Kenya atajitupa uwanjani kuwania medali ya dhahabu katika mbio za mita 800.

Brasilien Fußball WM Weltmeisterschaft 2014 Brasilien vs. Chile Neymar weint
Neymar nahodha wa BrazilPicha: picture-alliance/dpa/GES-Sportfoto

Rudisha aliitinga katika fainali jana , lakini wapinzani wake katika taji hilo ni pamoja na Wakenya wenzake Alfred Kipketer na Furguson Rotich.

Bingwa wa mbio za mita 200 Allyson Felix kwa upande wa wanawake ni nyota atakayeonekana katika mbio za mita 400 leo na Mfaransa Renaud Lavillenie anayeshikilia rekodi ya dunia anatetea taji lake la kuruka kwa upondo.

Nusu fainali soka

Kwa upande wa soka katika michezo ya Olimpiki wenyeji Brazil wanavaana na Honduras katika nusu fainali ya kwanza siku ya Jumatano na kisha Jumamosi Ujerumani na Nigeria wataoneshana kazi katika nusu fainali nyingine mjini Sao Paulo.

Wakati huo huo mahakama ya michezo ya dunia leo imeondolea mbali marufuku iliyowekwa na shirikisho la vyama vya riadha duniani IAAF dhidi ya Darya Klishna anayejuka juu dhidi ya kushiriki michezo ya Rio.

Russland Weitspringerin Darja Klischina
Darya Klishina wa UrusiPicha: Reuters/S. Karpukhin

Klishna , mwenye umri wa miaka 25 alikuwa ni Mrusi pekee aliyekubaliwa kushiriki michezo ya Rio lakini shirikisho hilo la michezo duniani lilimpiga marufuku siku ya Ijumaa baada ya taarifa mpya kuhusiana na rekodi yake katika masuala ya doping.

Baada ya siku moja ya kusikiliza kesi yake, mahakama ya upatanishi (CAS) alitangaza kwamba rufani ya Klishna imefanikiwa na ataendelea kushiriki mashindano hayo ya mjini Rio.

Wakati huo huo kamati ya Olimpiki ya michezo ya wenye ulemavu nchini Urusi imekata rufaa nyingine dhidi ya uamuzi wa kuipiga marufuku nchi hiyo kushiriki mashindano hayo ya wenye ulemavu mjini Rio kuhusiana na ushahidi kwa matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli kitaifa.

Deutschland Fußball Bundesliga FC Bayern München vs. Borussia Dortmund
Borussia Dortmund ikipambana na Bayern Munich katika Super CupPicha: Getty Images/Bongarts/O. Hardt

Super Cup Ujerumani

Bayern Munich iliishinda Borussia Dortmund jana Jumapili kwa mabao 2-0 katika kombe la Super Cup nchini Ujerumani ikiwa ni taji la kwanza kwa kocha mpya wa Bayern Carlo Anceloti, kombe ambalo mtangulizi wake Pep Guardiola aliyetimkia Manchester City msimu huu hakuweza kulitia mikononi kwa kipindi chote cha miaka mitatu aliyoishi mjini Munich akifunza Bayern Munich.

Ni mara ya tano kwa Bayern kulinyakua taji hilo mara hii , ikilingana sasa na Borussia Dortmund ambayo nayo hadi jana ilikuwa inaongoza katika kulinyakua kombe hilo ambalo hutumika pia kama la kufungua pazia la msimu wa ligi nchini Ujerumani.

Mashabiki walitarajia kumuona Mario Goetze akiichezea kwa mara ya kwanza tena Borussia Dortmund akitokea kwa mahasimu wao Bayern Munich lakini kocha Thomas Tuchel alimuacha katika benchi mchezaji huyo na mashabiki wengi walijiuliza kwanini ? Jibu alikuwa nalo kocha Thomas Tuchel.

Mario Goetze geht zurück zum BVB
Mario Goetze wa DortmundPicha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

"Kwasababu kama ilivyo kwa Raphael , Lucas Piszcek na Julian Weigl ambao wamefanya mazowezi kwa siku 9 tu na mchezo huu ni wa nguvu sana, na matayarisho hayakuwatosha."

Wachezaji ambao walikuja mwisho hawakuwa katika kiwango cha juu kwa ajili ya fainali hii, kuliko wachezaji waliokuwa katika mazowezi kwa wiki tano. Na ndio sababu ilikuwa kawaida kwetu kuwapa nafasi wachezaji hao.

Nae mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Lucas Podolski ametangaza kujiuzulu kutoka timu ya taifa. Nilimwambia kocha wa taifa kwamba kuanzia sasa sitacheza tena katika timu ya taifa amesema Podolski na kwamba anataka kupeleka nguvu zake sasa katika mambo mengine, kama familia yake.

Podolski aliichezea timu ya taifa kwa miaka 12, akiichezea timu hiyo mara 129 na kutawazwa bingwa wa dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Bundesliga Mainz gegen Dortmund
Kocha wa Dortmund Thomas TuchelPicha: Getty Images/AFP/D. Roland

Uhispania Super Cup

Nayo Barcelona ilipata ushindi wa mabao 2-0 jana dhidi ya sevilla katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa kombe la Super Cup nchini Uhispania ambapo mkondo wa pili utapigwa Jumatano.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger amesema wachezaji wake hawakuwa tayari kimwili kwa mchezo wa ufunguzi wa msimu wa ligi baada ya kusambaratishwa kwa mabao 4-3 dhidi ya Liverpool jana Jumapili.

Arsenal wanawatembelea mabingwa watetezi Leicester City siku ya Jumamosi na Wenger hana hakika iwapo baadhi ya wachezaji wake wa timu ya kwanza kama mlinzi wa kati Koscielny ama Per Mertesacker watakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo.

Kocha wa Liverpool anapigiwa upatu kuiongoza Liverpool kuwa moja kati ya timu zinazoweza kutoroka na taji la ubingwa wa Premier League msimu huu, lakini amesema ni mapema mno kuanza kufikiria kuhusu ubingwa.

Klopp alijilaumu kwa ukosefu wa uangalifu kwa wachezaji wake , na kusema alivyofurahia goli la Mane katika dakika ya 63 kuliwafanya wachezaji kuhisi kwamba tayari wamekwisha shinda.

Afrika: Champions League

Wydad Casablanca ya Morocco na Zesco United ya Zambia zimefanikiwa kuingia katika nusu fainali ya kombe la Champions League leo, baada ya Wydad kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas wa Cote d'Ivoire mjini Rabat.

Zesco United ya Zambia imejihakikishia kuingia nusu fainali baada ya kutoka sare ya mabo 2-2 mjini Cairo.

Zesco inaikaribisha Wydad Casablanca Agosti 24 ikihitaji ushindi ili kumaliza ikiwa katika nafasi ya kwanza na itakumbana na Zamalek ya Misri ama Enyimba ya Nigeria katika nusu fainali.

Omar Mahmoud Zamalek Ägypten Fussball
Omar Mahmoud wa Al-Zamalek ya MisriPicha: AFP/GettyImages

Mabingwa mara tano wa Afrika Zamalek wanaikaribisha Enyimba ya Nigeria nyumbani mjini Cairo baadaye leo Jumatatu ikihitaji pointi moja kujihakikishia nafasi ya pili katika kundi B nyuma ya Sundowns ya Afrika kusini.

Na kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo nasema kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / ape

Mhariri: Mohammed Khelef