1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatuhumu upinzani Syria kuhujumu mazungumzo

2 Machi 2017

Urusi imeushutumu ujumbe unaowakilisha upinzani wa Syria kwenye mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Geneva kwamba wanahujumu mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/2YXzm
Russland Die Sprecherin des Aussenministeriums Maria Zakharova
Picha: picture alliance/dpa/I. Pitalev

Huku tuhuma hizo zikitolewa, upinzani wenyewe umeelezea matarajio yao kwa utawala mpya wa Marekani katika kutatua mzozo uliodumu kwa takriban miaka sita nchini humo.

Matokeo ya siku ya kwanza ya majadiliano ya ndani, kama ilivyokuwa awali, yaliibua maswali kuhusiana na uwezekano wa wawakilishi wa upinzani wa Syria kufikia makubaliano, amesema msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni wa Urusi, Maria Zakharova.

Zakharova amesema, hatua ya kamati kuu ya majadiliano ya amani ya Syria,  kukataa kutoa ushirikiano kwa makundi mawili ambayo ni washirika wa Urusi kunamaanisha kwamba ni wazi inahujumu majadiliano yote yaliyohusisha ujumbe wa serikali ya Syria na makundi mengine ya upinzani.

Urusi ni mmoja wa washirika wakuu wa serikali ya Syria, ambaye anaendeleza kampeni yake ya mashambulizi ya angani kuvisaidia vikosi vya Bashar al-Assad

Kiongozi wa kamati hiyo ya HNC Nasr al-hariri amesema wana imani uongozi wa Trump utasaidia kudhoofisha nguvu ya Iran kwenye mzozo huo uliosababisha vifo vya takriban watu 310,000, na kuongeza kwamba kila mmoja anasubiri utawala huo mpya wa Marekani chini ya Rais Donald Trump kuingilia, huku wakishutumu vikali sera iliyoshindwa ya rais aliyepita Barack  Obama waliyoiita kuwa ni "janga".
 
Serikali ya Syria na upinzani wako Geneva tangu alhamisi iliyopita, lakini hawajawahi kuzungumza ana kwa ana, wakati ambapo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura akiwa katikati ya makundi hayo pinzani. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kumalizika ijumaa hii ama mwisho mwa wiki huku kukiwa na dalili finyu za mafanikio.

Schweiz Genf Staffan de Mistura
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura anayeongoza mazungumzo ya GenevaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Taarifa nyingine zilizotolewa na shirika la habari la Urusi, Interfax, zinasema Machi 9 mwaka huu, waziri wa masuala ya kigeni wa nchi hiyo, Sergei Lavrov atakutana na mwenzake wa Ujerumani Sigmar Gabriel mjini Moscow ambapo kwa pamoja watajadili mizozo inayokabili Ukraine na Syria. 

Huko nchini Syria, taarifa zilizotolewa na waangalizi zinasema jeshi la serikali pamoja na washirika wake wameendelea kuingia katikati ya mji wa Palmyra baada ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kuvirejesha nyuma vikosi vyake vingi kutoka maeneo ya ndani ya mji huo wa kihistoria.   

Kituo cha televisheni cha serikali kimearifu leo hii kwamba jeshi la serikali limeyashikilia maeneo yaliyoko mlima wa al-Tahr Kaskazini Magharibi mwa Palmyra.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman