1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yangojewa kuondosha majeshi yake Georgia

P.Martin19 Agosti 2008

Ulimwengu ungali ukingojea kujionea vikosi vya Urusi vikiondoshwa kutoka Georgia kama ilivyoahidiwa,huku serikali ya Tbilisi ikiituhumu Moscow kuwa imekiuka vibaya makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/F0n6
French Foreign Minister Bernard Kouchner, second right, gestures as U.S. Secretary of State Condoleezza Rice, left, talks with Greek counterpart Dora Bakoyannis, during an emergency NATO foreign minister meeting in Brussels, Tuesday Aug. 19, 2008. U.S. Secretary of State Condoleezza Rice and her NATO counterparts are reviewing relations with Moscow Tuesday and are expected to curtail high level meetings and military cooperation with Russia if it does not abandon crucial positions across Georgia. Person at right is OSCE Chairman Alexander Stubb. (AP Photo/Yves Logghe)
Waziri wa Nje wa Ufaransa Bernard Kouchner(pili kulia) akizungumza na waziri mwenzake wa Marekani Condoleezza Rice wakati wa mkutano wa dharura wa mawaziri wa nje wa NATO,mjini Brussels,Agosti 19,2008.Picha: AP

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Georgia,Shota Utiashvilli hakuna ishara yo yote kuwa Urusi inaondosha vikosi vyake. Badala yake,vikosi hivyo ndio vimejiimarisha katika vituo vilivyotekwa hapo awali ikiwa ni pamoja na eneo linaouzingira mji wa Gori ulioshuhudia mapigano makali.

Georgia ikiituhumu Urusi kuwa inasita kuondosha vikosi vyake imesema, operesheni za kijeshi zinazoendelea zinakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Georgia,Urusi inakwenda kinyume kabisa na masharti ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na marais wa Georgia,Ufaransa na Urusi.

Hata maafisa wa Kimarekani waliopo nchini Georia wamesema,baada ya mapigano kusitishwa katika katika Jimbo la Ossetia ya Kusini,Urusi ilipeleka zana za kurusha makombora ya masafa mafupi na hakuna ishara yo yote ya kurejesha nyuma majeshi yake ingawa siku ya Jumatatu Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitangaza kuwa itaanza kuviondosha vikosi vyake kutoka Georgia.Badala yake kuna ishara kuwa Urusi inaimarisha vikosi na zana za majeshi yake katika majimbo ya Ossetia ya Kusini na Abkhazia na hivyo kujiimarisha zaidi katika majimbo hayo mawili yaliyojitenga na Georgia.

Kwa upande mwingine,Rais wa Urusi Dmitry Medvedev amesema,Georgia imepaswa kuadhibiwa kwa sababu ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Ossetia ya Kusini iliyojitenga.Akaongezea kuwa Urusi itachukua kila hatua kuhakikisha usalama wa eneo hilo.Wakati huo huo Msaidizi wa Mkuu wa Majeshi ya Urusi,Anatoli Nogowizyn akaeleza kinagaubaga msimamo wa Urusi.Amesema:

"Nataka kusisitiza mara nyingine,kinachozungumza hapa ni kurejesha nyuma vikosi na sio kuondoa majeshi kuambatana na Mamlaka ya mwaka 1992 kuhusu vikosi vya amani.Hakuna mkataba mwingine halali."

Ni dhahiri kuwa matamshi kama hayo ni pigo kwa viongozi wa nchi za magharibi wanaoiona Georgia kama ni mhanga wa ushari wa Urusi.Kwani kuambatana na makubaliano ya amani yaliyotiwa saini chini ya upatanishi wa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa rais katika Umoja wa Ulaya,vikosi vya Georgia vinapaswa kurejea kambini na vikosi vya Urusi navyo viondoke eneo hilo.Kikosi kidogo tu cha Urusi ndio kinachopaswa kubakia ndani na ukingoni mwa Ossetia ya Kusini na Abkhazia.Lakini Georgia ina wasi wasi kuwa Urusi huenda ikaitumia fursa hiyo kukalia maeneo yaliyojitenga.

Ukweli ni kwamba,washirika wa magharibi hawana turufu nzito mezani dhidi ya Urusi,nchi iliyo na utajiri mkubwa wa mafuta.Juu ya hivyo,mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za NATO wanaokutana Brussels kwa kikao cha dharura,wamekubaliana kuishinikiza zaidi Moscow kuondoa vikosi vyake huko Georgia.