1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yasimamisha mashauriano na Urusi.

Krause Hermann20 Agosti 2008

Nchi za mfungamano wa kijeshi wa NATO zimesimamisha mashauriano yanayofanywa mara kwa mara na Urusi kwa sababu ya mgogoro wa Georgia.

https://p.dw.com/p/F1Vg
Katibu Mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer.Picha: AP

Nchi za mfungamano wa kijeshi wa NATO zimesimamisha mashauriano yanayofanyika mara kwa mara na Urusi kutokana na mgogoro wa Georgia.

Nchi hizo zimepitisha uamuzi huo wakati ambapo vyombo vya habari vimeripoti kuwa majeshi ya Urusi sasa yameanza kuondoka kwenye ardhi ya Georgia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters ,malori ya kijeshi yamevuka mpaka wa Georgia na kurejea nchini Urusi. Mwandishi wa shirika hilo ameripoti habari hizo kutoka mji wa Verkhny Zaramag.

Nchi za magharibi zimekuwa zinaitaka Urusi iondoe majeshi yake yaliyoivamia Georgia.

Ripota wa shirika la Reuters amesema ameyaona magari hayo makubwa ya kijeshi yakianza kuondoka na kuvuka mpaka na kuingia Urusi. Ripota huyo alikuwa kwenye mpaka wakati magari hayo kadhaa yalipokuwa yanarudi nyumbani.

Urusi yenyewe imesema kuwa hadi kufikia ijumaa itakuwa imeshaondoa majeshi yake ,kutoka Georgia lakini pia imesema itabakiza wanajeshi 500 katika jimbo la Ossetia ya kusini ili kuimarisha usalama.

Kwa mujibu wa makubalinao ya vipengere sita yaliyofikiwa kutokana na usuluhishi wa Umoja wa Ulaya, Urusi itaendelea kuwa na wanajeshi katika jimbo hilo.

Hatahivyo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za mfungamano wa NATO wameamua kusimamisha ushirikiano na Urusi .

Juu ya uamuzi huo mjumbe maalumu wa Urusi kwenye mfungamano wa NATO Dimitri Ragozin amesema haoni iwapo patatokea mfarakano mkubwa baina ya nchi yake na nchi za NATO.