1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zaanza tena mazungumzo

Aboubakary Jumaa Liongo1 Juni 2009

Urusi na Marekani zimeanza duru mpya ya mazungumzo kati yao kuangalia uwezekano wa kufikiwa kwa mkataba mpya wa upunguzaji silaha za nuklia.

https://p.dw.com/p/I1ZF
START I Abkommen 1991
Marais wa zamani wa Marekani na Urusi, George Bush na Mikhael Gorbachev mwaka 1991 wakitia saini makubaliano ya mkataba wa STARTPicha: picture-alliance/dpa

Mkataba huo mpya unatarajiwa kuchukua nafasi ya ule uliyopo sasa ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.


Wajumbe wa pande zote mbili wameanza siku hii ya kwanza ya duru hiyo ya mazungumzo yao katika ofisi za ubalozi wa Urusi mjini Geneva kwa mazungumzo ya ndani.


Mwanadiplomasia mmoja wa Urusi amesema kuwa ujumbe wa Marekani uliwasili katika ofisi hizo milango ya saa sita mchana kwa saa za Afrika Mashariki, kwa ajili ya duru hiyo ya pili ya mazungumzo.


Maafisa wa pande zote mbili wamesema kuwa ni masuala machache tu yatakayojitokeza katika mazungumzo hayo ya siku tatu, ambayo ni matayarisho ya mkutano wa kilele kati ya nchi hizo mbili unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 mwezi huu.


Barack Obama vor einem Computerbildschirm
Rais Barack ObamaPicha: AP / DW-Montage

Matokeo ya mazungumzo ya mwanzo yaliyofanyika mnamo wiki mbili zilizopita mjini Moscow, yanatarajiwa kutangazwa na Rais Barack Obama na Rais Dmitry Medvedev watakapokutana katika mji mkuu wa Urusi Moscow.


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ian Kelly akizungumza mjini Washngton juu ya kile kinachojadiliwa, amesema kwa sasa si muda muafaka wa kutangaza kwa kina kinachojadiliwa.


Makubaliano ya kuanza kwa mazungumzo ya kufikia mkataba wa kuzuia silaha za nuklia ni hatua kubwa iliyo dhahiri ambayo imefikiwa katika kuurejesha uhusiano kati ya Marekani na Urusi ambayo imechukuliwa na utawala wa Rais Obama.


Lakini hata hivyo bado hatua hiyo inakwanzwa na mpango wenye utata wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami katika Ulaya Mashariki, mpango ambao umeiudhi Urusi.


Sergei Lavrov Hillary Clinton
Bibi Hillary Clinton, kulia na Waziri mwenziye wa nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: AP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton wakati alipokutana kwa mara ya kwanza na waziri mwenziye wa nje wa Urusi Sergei Lavrov mjini Geneva mwezi March alimnyooshea mkono uliyokuwa na mpango wa kuanza tena kwa mazungumzo ya kufikiwa kwa mkataba mwengine wa uzuiaji silaha za nuklia.


Mkataba uliyopo sasa ambao ulitiwa saini mwaka 1991 muda mfupi kabla ya kuanguka kwa uliyokuwa muungano wa kisoviet, unazitaka pande zote mbili Urusi na Marekani kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha silaha za nuklia inazozimiliki.Mkataba huo unamalizika tarehe 5 Decemba mwaka huu.


Lakini wadadisi na wafuatiliaji wa siasa za nchi hizo hawaoni kama kuna uwezekano wa kuwepo na mabadiliko.


Mwezi uliyopita Waziri wa Nje wa Urusi Sergei Lavrov alielezea dhamira ya nchi yake kuona kuwa suala la mpango wa Marekani kuweka makombora Ulaya Mashariki linajadiliwa katika mazungumzo hayo.


Lakini maafisa wa Marekani wamekuwa wakisisitiza kuwa, pamoja na kwamba wako tayari kulijadili suala hilo, lakini siyo ndani ya mazungumzo juu ya kufikiwa kwa mkataba huo mpya wa kuzuia nuklia.


Rais Obama ameagiza kupitiwa upya kwa mpango huo wa kutaka kuweka makombora ya kujihami katika Ulaya Mashariki, ambao Marekani imesisitiza kuwa una nia ya kukabiliana na kitisho cha Iran.


Makombora hayo baadhi yatawekwa katika nchi ambazo zinapakana na Urusi, hatua ambayo Moscow imesema ni hatari kwa usalama wake.


Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman