1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zapinga kuiwekea vikwazo Syria

Yusra Buwayhid
1 Machi 2017

Urusi na China zimepinga kuiwekea Syria vikwazo vya Umoja wa Mataifa kupitia kura ya turufu. Urusi imesema hakuna ushahidi wa kutosha wa kufanya hivyo. Marekani imelaani vikali hatua hiyo ya Urusi na China.

https://p.dw.com/p/2YQIX
UN Sicherheitsrat in New York
Picha: Reuters/M. Segar

Uchunguzi wa pamoja kati ya Umoja wa Mataifa pamoja na shirika la kufuatilia utumiaji wa silaha za kemikali umedhihirisha kuwa, serikali ya Syria ilifanya mashambuluzi matatu ya kutumia gesi ya klorini na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislam IS wamefanya shambulio moja la kutumia gesi ya haradali. Balozi wa Marekani kwa umoja huo, Nikki Haley, amezituhumu nchi zote mbili kwa kushindwa kuiwajibisha serikali ya Rais wa Syria Bashar al-Asaad kwa kutumia silaha za kemikali hata baada ya uchunguzi kuthibitisha.

"Uchunguzi uliofanywa hauna tatizo lolote. Urusi haitaki tu kuukosoa utawala wa Assad kwa kosa la kutumia silaha za kemikali. Huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo ujumbe gani tunauonesha ulimwengu? Ukiwa mshirika wa China na Urusi watawatetea marafiki zao hata ambao wanatumia silaha za kemikali kuua raia wao wenyewe. Wengine wanasema kuwa tunapaswa kuzingatia zaidi juu ya IS. Marekani inalaani matumizi yoyote ya silaha za kemikali, iwe kundi la au mtu mwingine yoyote," amesema Nikki Haley.

UN Sicherheitsrat in New York
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjini New YorkPicha: Reuters/M. Segar

Rasimu ya azimio hilo ilikuwa na nia ya kupiga marufuku biashara ya helikopta kwa serikali ya Syria, na ingewawekea vikwazo vya kiuchumi pamoja na usafiri baadhi ya maafisa wa kijeshi na wa serikali ya Syria.

Azimio hilo limeandaliwa baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na Shirika linalopiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali (OPCW). Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa vikosi vya serikali ya Syria vilitumia helikopta kutupa mabomu ya mapipa yenye gesi ya klorin.

Nchi tisa ziliunga mkono kwa kulipigia kura azimio hilo la Braza la Usala lililowasilishwa na Uingereza, Ufaransa, na Marekani. Nchi tatu zimelipinga azimio hilo ikiwa ni pamoja na Urusi, China na Bolivia. Kazakhstan, Ethiopia na Misri hazikupiga kura kabisa. 

Ili azimio la Umoja wa Mataifa lipitishwe katika baraza la Usalama, kwa kawaida linahitaji kura tisa za kuliunga mkono bila ya kupingwa na nchi zenye uwezo wa kutumia kura ya turufu ambazo ni Marekani, Ufaransa, Urusi, Uingereza na China.

Syria kwa upande wake imekana kuhusika na utumiaji wa gesi ya kemikali dhidi ya watu wake. Naibu balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Mounzer Mounzer ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa serikali ya Syria inapinga utumiaji wa silaha za maangamizi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/dw

Mhariri: Iddi Ssessanga