1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zapinga azimio la UN kuhusu Syria

Grace Kabogo
6 Desemba 2016

Urusi na China zimepiga kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatotaka kuwepo kwa mpango mpya wa kusitisha mapigano Aleppo, Syria.

https://p.dw.com/p/2Tnpq
Wladimir Putin und Wen Jiabao
Picha: picture-alliance/dpa/A. Maltsev

Azimio hilo linalopendekezwa na Misri, Uhispania na New Zealand, linazitaka pande zote zinazohasimiana kusitisha mashambulizi kwenye mji wa Aleppo ili kupisha zoezi la kupelekwa misaada ya kibinadamu kwenye mji huo. Hata hivyo, Urusi mshirika wa karibu wa Rais wa Syria, Bashar al-Assad, ilielezea wasiwasi wake kuhusu kura hiyo na ilitaka ifanyike leo ili kutoa muda kwa maafisa wa Marekani na Urusi kukutana mjini Geneva, Uswisi na kuzungumzia jinsi ya kuwaondoa waasi waliobakia Aleppo.

Mazungumzo hayo ya leo yatahusu mpango wa kuwaruhusu waasi katika mji huo uliozingirwa kuondoka, lakini mpango huo unapingwa na vikosi vya upinzani nchini Syria. Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema Marekani na Urusi ziko karibu kufikia makubaliano kuhusu masuala muhimu.

Russland und China blockieren UN-Resolution zu Feuerpause in Aleppo
Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kuraPicha: picture-alliance/Photoshot

''Kama tunavyojua, mipango kama hii ya kusitisha mapigano, imekuwa ikitumiwa na wapiganaji  kuongeza uasi na kuimarisha maeneo yao, hatua itakayowaumiza zaidi raia. Urusi haiwezi kuunga mkono rasimu ya azimio hili lililopendekezwa na nchi hizo tatu zenye kutoa misaada ya kibinaadamu,'' alisema Churkin.

Marekani: Urusi inatafuta tu sababu

Hata hivyo, Marekani imesema Urusi inatumia kisingizio hicho kama sababu ya kulikataa tu azimio hilo la Umoja wa Mataifa. Balozi msaidizi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Michele Sison, amesema Urusi inalenga kulinda maslahi yake ya kijeshi, badala ya kuwasaidia raia wa Aleppo. Sison amesema wataendeleza mazungumzo na Urusi kuhakikisha wanawaondolea mateso watu wa Aleppo.

Akifafanua zaidi, Sison amesema ''ngoja niwaambie kile ambacho Urusi na China wamekifanya hii leo. Wamepiga kura kuzuia azimio na kuruhusu mashambulizi kuendelea mashariki mwa Aleppo. Wamepiga kura ya turufu kupinga kupelekwa dawa kwa watu ambao watakufa bila kuzipata, kuondolewa wagonjwa, kupelekwa chakula kwa watu wanaokabiliwa na njaa pamoja na kuyaokoa maisha ya raia wa Syria wasio na hatia.''

Syrien Kämpfe in Aleppo
Askari wa Syria akiweka bendera ya taifa ya Syria kwenye eneo la Ramouseh, AleppoPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Venezuela nayo ilipiga kura ya turufu kulipinga azimio hilo, huku Angola ikiwa haijapiga kura. Wanachama wengine 11 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, walipiga kura kuliunga mkono azimio hilo.

Hayo yanajiri wakati ambapo waasi wamekataa kuondoka Aleppo huku majeshi ya serikali yakizidi kusonga mbele. Abu Abdel Rahman al-Hamawi kutoka moja ya makundi ya waasi la Jeshi la Kiislamu, amesema wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho. Vikosi vya jeshi vinavyomtii Rais al-Assad anayeungwa mkono na Urusi, vinadhibiti theluthi-mbili ya mji huo tangu katikati ya mwezi Novemba.

Wakati huo huo, wauguzi wawili wa Urusi na raia wanane wameuawa jana katika shambulizi la kombora lililofanywa na waasi mjini Aleppo. Shambulizi hilo lilikuwa likiyalenga maeneo yanayodhibitiwa na serikali magharibi mwa Aleppo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA
Mhariri: Josephat Charo