1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2018, Qatar 2022

2 Desemba 2010

Wajumbe wa kamati tendaji ya shirikisho la kandanda duniani FIFA leo wametoa uamuzi muhimu katika soka kwa kuichagua Urusi kuwa taifa litakalokuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia kwa mwaka 2018 kwa mara ya kwanza

https://p.dw.com/p/QOHM
Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: AP

Rais wa shirikisho la soka duniani, FIFA, Sepp Blatter ameitangaza Urusi kuwa mwenyeji wa michuano ya kuwania kombe la kandanda la dunia mwaka 2018, huku Qatar akichaguliwa kuyaandaa mashindano hayo mwaka 2022.

Wajumbe 22 wa kamati tendaji ya shirikisho hilo la kandanda duniani FIFA wamesikiliza maelezo ya nusu saa kutoka kwa kila kila nchi iliyo toa ombi lake kwa ajili ya kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2018 katika kinyang'anyiro ambacho wadadisi wanasema ni cha vuta nikuvute.

Tangazo la nchi gani imeshinda kuwa mwenyeji wa fainali hizo limetolewa na rais wa FIFA Sepp Blatter hii leo (02.12.2010) katika kituo cha maonyesho mjini Zurich. Pia ameitangaza Qatar kuwa mshindi kati ya washindani watano waliowania kuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2022, nchi ambazo zilitoa maelezo yao jana Jumatano.

Uingereza na Urusi pamoja na maombi mawili ya nchi mbili kwa pamoja Uholanzi na Ubelgiji na Hispania na Ureno , ziliwania kuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2018, wakati Australia, Japan, Katar, Korea ya kusini na Marekani ziliwania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2022.

Uingereza na Urusi, zilionekana kuwa nchi zenye uwezo mkubwa wa kushinda uteuzi huo kwa ajili ya fainali za mwaka 2018, na zote zilipata pigo kidogo katika kampeni zao.

Kuzuka kwa ghasia katika soka katika mchezo wa kuwania kombe la chama cha soka nchini Uingereza, mjini Birmingham siku ya Jumatano kumerejesha fikra mbaya za uhuni katika michezo hali ambayo imeukumba mchezo huo wa soka nchini Uingereza katika miaka ya 1980. Moja kati ya kampeni zake kuu katika kinyang'anyoro hicho ni kwamba hali hiyo ya uhuni na ghasia katika michezo imetoweka katika mchezo huo nchini humo.

Urusi nayo ilipata pigo wakati waziri mkuu Vladimir Putin alipotangaza hatakwenda mjini Zurich kujitokeza pamoja na kikosi kinachoitangaza Urusi katika kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2018, kwa kile alichokiita, ushindani usio sawa, akiwa na maana madai katika vyombo vya habari vya Uingereza kuhusu rushwa dhidi ya baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji ya FIFA.

Mwandishi: Sekione Kitojo / RTRE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman