1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yaichapa Korea ya Kaskazini 7:0 na Chile yavunja tumbuu ya lango la Uswisi 1:0

21 Juni 2010

Je, Ivory Coast kufuata nyayo ya Kameroun kurudi nyumbani ?

https://p.dw.com/p/NzRn
Cristiano Ronaldo aichapa Korea kaskazini mabao 7:0.Picha: AP

Chile baada ya kupiga hodi nyingi katika lango la Uswisi, mwishoe, ilivunja tumbuu ya lango la Uswisi na kuikomea bao 1:0. Uswisi, ikicheza na wachezaji 10 tu tangu kipindi cha kwanmza wakati mwingi ikijilinda.Kwa ushindi wa Chile, leo na Paraguay jana, timu zote 5 za Amerika Kusini na kati,zinaelekea duru ya pili ili kutoa changamoto kwa timu za ulaya.

Hapo kabla, Ureno, iliichezesha Korea ya Kaskazini ,kindumbwe-ndumbwe na kuizaba mabao 7:0 na kutia mguu mmoja duru ijayo.Korea ya kaskazini , imeshafungishwa virago iage Kombe la Dunia.Brazil ikiwa imeshakata tiketi yake ya duru ya pili hapo jana ilipoitoa Ivory Coast kwamabao 3:1, kikosi cha nahodha Didier Drogba, takriban hakina tena nafasi ya kucheza duru ya pili,isipokuwa ifanye juju- miujiza ya dimba.

Mkondo wa mchezo uligeuka kwa mabao 3 ya haraka kipindi cha pili kutoka kwa Simao,Hugo Almeida na Tiago.Halafu nahodha Cristano Ronaldo, akatia bao la 6 kabla ya Tiago kuridi tena kupiga msumari wa 7 katika jeneza la Korea ya kaskazini na kuizika kabisa katika kaburi la FIFA iliochimbiwa Cape Town.

Mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil, jana wamekata tiketi yao ya duru ya pili ya kombe la dunia ,mpambano ambao uligubikwa na patashika uwanjani iliopelekea kutimuliwa nje ya chaki ya uwanja kwa stadi wa Brazil Kaka.

Kocha Eriksson alisema:

"Bao la kwanza la Brazil,lilikuwa maridadi kabisa.Nilitumai timu yangu ingelifufuka baada ya kuchapwa mabao 3,lakini , hatukuweza na kwa bahati mbaya,hatukuweza kutia zaidi ya bao 1."

Timu 4 za Afrika kati ya 6 zilizotazamiwa kulifanya Kombe la kwanza la Dunia barani Afrika 2010, ni la kukumbukwa, zinaburura mkia katika makundi yao na ziko njiani kufunga virago na kuondoka:Afrika kusini, iko nafasi ya 4 na ya mwisho ya kundi lake A kabla haikucheza na Ufaransa,iliokumbwa na misukosuko.Nigeria, halkadhalika, ikiwa katika kundi B, ni ya mwisho .Isitoshe, Algeria, ilioipiga kumbo Misri, mabingwa wa Afrika,wanaburura mkia licha ya kuwatoa jasho waingereza n a kumudu sare ya 0:0 na mbaya zaidi, simba wa nyika-Kameroun, hawakunguruma na ni wa kwanza kuaga kombe la dunia porini mwao.

Leo ni zamu ya mabingwa wa ulaya-Spain, kufuta madhambi yao waliofanya walepocheza na Uswisi.Spain lazima ishinde leo kuweka hayi matumaini iliowekewa kuwa huu ni mwaka wao.Kuteleza katika mpambano wao wa kwanza si kuangika.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE

Uhariri: Abdul-Rah