1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yafuzu kwa fainali Euro 2016

7 Julai 2016

Cristiano Ronaldo ameng'ara katika mtihani wa kuamua nani mkali kati yake na Gareth Bale, kwa kuingiza goli la kwanza na kutoa pasi iliyosaidia la pili katika mechi ya kwanza ya nusu fainali euro 2016.

https://p.dw.com/p/1JKsz
Ronaldo yaisaidia timu yake ya taifa kufuzu kwa mechi ya fainali Euro 2016
Ronaldo yaisaidia timu yake ya taifa kufuzu kwa mechi ya fainali Euro 2016Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ureno imetinga fainali ya kombe la ubingwa wa mataifa ya Ulaya, Euro 2016 baada ya kuizima ndoto ya Wales kwa kuilambisha magoli mawili kwa sufuri mjini Lyon, Ufaransa. Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali iliyopigwa usiku wa kuamkia leo ilikuwa imechukuliwa kama kipimo cha nani mkali kati ya washambuliaji wawili wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo wa Ureno, na Gareth Bale wa Wales.

Ni Ronaldo aliyeng'ara hasa katika ngwe ya pili ya mechi. Ilikuwa mnamo dakika ya 50 ya mchezo alipopaa kimo cha zaidi ya mita 2.5 na kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliofyatuka na kutua wavuni, ukimwacha mlinda mlango wa Wales Wayne Hennesey akiduwaa.

Wakati wachezaji wa Wales wakitafakari kilichowakuta na kujaribu kujipanga upya, kwa mara nyingine Ronaldo alionyesha kuwa nyota yake siyo ya kubabaisha, kwa kupenyeza pasi iliyotua kwenye mguu wa Nani na kubadilishiwa mkondo, na kwa mara ya pili katika muda wa dakika tatu, kipa Hennesey akajikuta akigeuka kuokota mpira wavuni.

Hatimaye machozi ya furaha?

Akizungumza baada ya mechi hiyo Ronaldo amesema kikosi kizima cha Ureno kimefanya kazi murua kufuzu kwa mechi ya fainali, na kuongeza kuwa anayo matumaini kuwa baada ya mechi hiyo atalia machozi ya furaha, sio ya huzuni kama ilivyotokea mwaka 2004 waliposhindwa na Ugiriki kwenye uwanja wa nyumbani mjini Lisbon.

''Mara zote nimesema nataka kubeba kombe na timu ya taifa ya Ureno'' amesema Ronaldo, na kuongeza, ''nimekuwa katika kiwango cha juu kwa miaka 13, na takwimu kamwe hazidanganyi'', amemalizia.

Pamoja na kufungasha virago kurejea nyumbani, Wales wanaondoka kifua mbele, kwa kuweza kucheza nusu fainali, ikiwa ndio kwanza wameshiriki katika mashindano ya kimataifa kwa muda wa miaka 40.

Licha ya kuyaaga mashindano, Wales wameridhika na hatua waliyoipiga
Licha ya kuyaaga mashindano, Wales wameridhika na hatua waliyoipigaPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Gareth Bale amesema na hapa manukuu, ''Tumefanya kila tulichoweza, uwanjani na nje ya uwanja. Tungependa kuwashukuru mashabiki wetu, ambao wamekuwa mfano wa kuigwa'', mwisho wa kumnukuu.

Pengo la Ramsey, Pepe ladhihirika

Mechi kati ya timu hizo ilikuwa imeanza kwa tahadhari, pengine kwa sababu kila upande ulimkosa mchezaji muhimu. Wales haikuwa na huduma za kiungo wake, Aaaron Ramsey ambaye alitumikia adhabu baada ya kupewa kadi mbili za njano, na Ureno ilimkosa nondo katika safu ya ulinzi Pepe, ambaye alikuwa na majeraha.

Mechi hii ilikuwa ya kwanza kati ya sita kwa Ureno kuishinda katika muda wa kawaida wa dakika tisini tangu mashindano haya yalipoanza nchini Ufaransa.

Ronaldo ambaye anashikilia rekodi kama mchezaji aliyeingiza magoli mengi katika michuano ya Champions League, hivi sasa yuko sambamba na Michel Platini wa Ufaransa kwa kufunga magoli mengi katika fainali za ubingwa wa Ulaya, kila moja akiwa na magoli 9.

Ureno ambayo tayari inayo tiketi kibindoni itasubiri mshindi kutoka mechi nyingine ya nusu fainali itakayochezwa leo kati ya wenyeji Ufaransa na Ujerumani kwenye uwanja maarufu wa Velodrone mjini Marseilles.

Habari njema kwa Ujerumani ni kwamba Nahodha wa timu Bastian Schweinsteiger yuko fiti kwa mechi ya leo, ingawa Sami Khedira na Mario Gomez wana majeraha, naye beki Mats Hummels anatumikia adhabu. Ufaransa kwa upande wake, kikosi kizima kimekamilika.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/afpe