1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno na Uhispania zatoka sare katika mechi kali

Bruce Amani
16 Juni 2018

Cristiano Ronaldo amedhihirisha wazi kuwa yeye ndiye jogoo wa mjini katika Kombe la Dunia baada ya kufunga hat trick na kuisaidia Ureno kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu na Uhispania

https://p.dw.com/p/2zfJq
Fußball WM 2018 Portugal - Spanien
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Nyota huyo wa Real Madrid alisukuma wavuni bao tamu kupitia mkwaju wa freekick katika dakika ya 88 na kuwapa pointi moja mabingwa hao wa Ulaya katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi B, baada ya bao la kipipindi cha pili la Nacho kuwaweka Uhispania kifua mbele mabao matatu kwa mawili. Kabla ya hapo CR7 alikuwa ameipa timu yake uongozi katika kipindi cha kwanza kupitia mkwaju wa penalty baada ya kuangushwa katika eneo la hatari, kabla ya Diego Costa kusawazisha kwa kuwabwaga mabeki watatu wa Ureno na kufunga bao safi.

Ronaldo sasa ni mchezaji wan ne kufunga katika mashindano manne ya Kombe la Dunia, akifuata nyayo za Pele na Wajerumani Miroslav Klose na Uwe Seeler.

Fußball WM 2018 Portugal - Spanien Trainer Fernando Hierro
Kocha wa Uhispania Hierro hakuamini macho yakePicha: Reuters/H. McKay

Ureno kisha walifunga tena baada ya Ronaldo kusukuma wavuni kombora ambalo lilimzidi maarifa kipa wa Uhispania David de Gea ambaye aliutema mpira.

Katika kipindi cha pili Uhispania walijipanga upya na kusawazisha kupitia Costa ambaye alitikisa wavu baada ya kuandaliwa assist ya kichwa kutoka kwa Sergio Ramos kutokana na mpira wa freekick.

Katika mechi ya kwanza ya siku, beki wa Uruguay Jose Jimenez alifunga bao la kichwa katika dakika ya 89 wakati Wamerika Kusini hao wakiibwaga Misri ambayo ilikosa sana huduma za mchezaji wao nyota Mo Salah. Salah alikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba huku kocha wake akisema kuwa atacheza mechi inayofuata. Ushindi wa Uruguay unawaweka wao na Urusi katika usukani wa Kundi A na pointi tatu kila mmoja.

Katika mechi nyingine ya Kundi B jana, wachezaji wa Iran walivamia uwanjani baada ya mchezo kumalizika kana kwamba wameshinda Kombe la Dunia. Walikuwa wakishangilia pointi tatu ambapo Aziz Bouhaddouz wa Morocco alijifunga katika lango lake na kuwapa ushindi wa bao moja kwa bila.

Weltmeisterschaft - Gruppe B - Marokko gegen den Iran
Majonzi kwa wachezaji wa Morocco Picha: Reuters/P.Olivares

Katika mechi za leo, itakuwa zamu ya Lionel Messi ambaye atashuka dimbani wakati Argentina inafungua mechi za kundi D dhidi ya Iceland, taifa dogo kabisa kuwahi kucheza katika Kombe la Dunia.

Nyota huyo anashiriki katika kinyang'anyiro cha mwaka huu chini ya shinikizo kubwa cha hatimaye kushinda taji la kimataifa. Wakosoaji wa mshambuliaji huyo wa Barcelona wanaamini kuwa pengo hilo linamuondoa kwenye mjadala wa kuwa mchezaji bora katika historia ya kandanda. Messi anacheza katika Kombe lake la nne la Dunia na alitinga fainali mwaka wa 2014 na kuondolewa na mabingwa Ujerumani.

Ufaransa itachuana na Australia katika mechi ya Kundi C uwanjani Kazan Arena. Ufaransa ina kikosi kikali sana kikiongozwa na kiungo mshambuliaji Antoine Griezmann. Kwa upande wa Australia, Tim Cahill anajaribu kujiunga na Pele na washambuliaji wa zamani wa Ujerumani Miroslav Klose na Uwe Seeler na sasa Cristiano Ronaldo kama wachezaji pekee waliowahi kufunga bao katika mashindano manne ya Kombe la Dunia.

Peru itashuka dimbani dhidi ya Denmark katika mechi ya Kundi C. Denmark haijashindwa mechi yoyote katika miezi 18 ikiongozwa na kiungo wa Tottenham Christian Eriksen. Katika mechi ya Kundi D Croatia na Nigeria zitakwaruzana. Croatia ilitinga nusu fainali miaka 20 iliyopita nchini Ufaransa na inashiriki kwa mara yake ya tano katika Kombe la Dunia. Timu hiyo ina vipaji kama vile Luka Modric, Ivan Rakitic na Mario Mandzukic.

Nigeria ina kikosi change Zaidi katika Kombe la Dunia mwaka huu lakini kina wachezaji kadhaa wa Ligi ya Premier wakiwemo Alex Iwobi, Wilfried Ndidi na Victor Moses.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef