1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Zimbabwe walalamika kuchelewa kwa matokeo

Charo, Josephat31 Machi 2008

Matokeo kuanza kutangazwa leo

https://p.dw.com/p/DXao
Wazimbabwe wakitazama matokeo ya awali yaliyobandikwa ukutani katika kitongoji cha Mbare mjini HararePicha: AP

Upinzani nchini Zimbabwe umewalaumu maafisa wa tume ya uchaguzi kwa kuyachelewesha makusudi matokeo ya uchaguzi katika hatua ya mwisho ya kumsaidia rais Robert Mugabe aendelee kubakia madarakani.

Huku tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ikisema itayatangaza matokeo ya kwanza leo asubuhi, chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, kimesema imebainika wazi kwamba rais Mugabe ameshindwa na hakitakubali matokeo yatakayokwenda kinyume na ukweli huo.

Wanachama wa chama hicho wanahofu chama tawala wa ZANU-PF kinatumia wakati huu kuyabadilisha matokeo ya uchaguzi uliofanyika juzi Jumamosi nchini humo. Kiongozi wa chama cha MDC, bwana Morgan Tsvangirai amedai ameshinda uchaguzi huo kulingana na ripoti za matokeo ya awali. Hata hivyo rais Mugabe amesema anaamini amewashinda wapinzani wake katika uchaguzi huo.

Hali ya wasiwasi imezidi katika mji mkuu Harare na polisi wamekuwa wakishika doria kwenye barabara zote za mji huo.