1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wamshinda rais Sarkozy katika uchaguzi wa Ufaransa

Charo,Josephat10 Machi 2008

Chama cha kisoshalisti kimeshinda awamu ya kwanza ya uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa

https://p.dw.com/p/DLhG
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akipiga kura katika uchaguzi wa baraza la mji mkuu ParisPicha: AP

Chama cha kihafidhina cha UMP cha rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, kimepata pigo katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa uliofanyika jana nchini humo. Hata hivyo chama hicho kimefaulu kukwepa kushindwa kwa idadi kubwa ya kura kama ilivyokuwa imebashiriwa katika matokeo yanayoonekana kuwa onyo kwa utawala wa rais Nicolas Sarkozy. Chama cha upinzani cha Socialist nchini Ufaransa kinatarajiwa kushinda awamu ya pili ya uchaguzi baada ya kushinda awamu ya kwanza ya uchaguzi wa jana wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha chama cha wasoshalisti kimeshinda uchaguzi katika mji wa pili mkubwa nchini Ufaransa wa Lyon na kinaonekana kuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi wa mji mkuu Paris katika awamu ya pili ya uchaguzi utakaofanyika tarehe 16 mwezi huu. Ikiwa mkondo utaendelea kuwa hivi chama cha kisoshalisti kitaichukua miji 30 iliyopoteza kwa chama cha Union for a Popular Movement, UMP, cha rais Sarkozy.

Awamu ya kwanza imetajwa kuwa onyo na gazeti la Le Parisien, huku lakini kukiwa na mengi ya kushindaniwa katika miji kadhaa ya Ufaransa. Viongozi wa upinzani wamewatolea mwito wafuasi wao wajitokeze kwa wingi wikendi ijayo kupiga kura ili kuubadili ushindi wa awali kuwa ushindi kamili dhidi ya chama tawala cha rais Sarkozy.

Kiongozi wa chama cha Socialist, Francois Hollande, amesema kila kitu bado kiko wazi na hakuna kilichoshindwa wala kupotezwa. Aidha kiongozi huyo amesema matokeo yana lengo la kumpa somo rais Sarkozy na serikali yake kwa sera zake ilizoziendesha katika kipindi cha miezi tisa.

Uchaguzi ni mtihani wa kwanza kwa Sarkozy

Uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa ni mtihani wa kwanza kwa rais Nicolas Sarkozy tangu alipoingia madarakani miezi kumi iliyopita. Uchaguzi huo pia unafanyika wakati umaarufu wa rais Sarkozy ukiwa umeshuka.

Ingawa rais Sarkozy alichaguliwa kwa kuahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi, wapigaji kura wengi wanahisi ametumia muda wake mwingi kwa maisha yake binafsi, na kumuoa mwimbaji mashuhuri, Carla Bruni, baada mapenzi ya kimbunga.

Katika ngazi ya kitaifa, vyama vya upinzani vimeshinda asilimia 47.94 ya kura zilizopigwa jana huku vyama vya mrengo wa kati na kulia vikipata asilimia 45.49, ushindi ambao ni kinyume na matarajio ya baadhi ya wachambuzi wa kisiasa waliobashiri kabla awamu ya kwanza ya uchaguzi kufanyika kwamba upinzani ungepata ushindi wa kishindo. Idadi ya wapigaji kura waliojitokeza inakadiriwa kufikia asilimia takriban 65.

´Ni athari isiyotarajiwa ya kura za maoni. Unajikuta ukiamini utapata ushindi mkubwa, lakini jambo hilo halitokei na unakuwa katika hali ya kuvunjika moyo licha ya kupata ushindi,´ imesema taarifa ya chama cha Liberation kinachoegemea mrengo wa kushoto katika uhariri wake.

Kinyang´anyiro kitakuwa kikali

Maeneo yanayotazamiwa kushuhudia mashindano makali katika uchaguzi wa Jumapili ijayo ni miji ya kusini mwa Ufaransa ya Marseille na Toulouse, na mji wa mashariki wa Strasbourg. Miji hii yote inadhibitiwa na serikali lakini huenda ikaanguka mikononi mwa wasoshalisti.

Pande zote mbili za serikali na upinzani zinakabiliwa na kibarua kigumu cha mashauriano kujaribu kupata mikataba na maeneo ya mashinani huku chama cha Democratic Movement, MODEM, mara kwa mara kikishikilia mizani ya madaraka.

Kiongozi wa chama cha MODEM, Francois Bayrou, aliyeshikilia nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana, amekataa kuunga mkono upande wowote na kumshauri rais Sarkozy asiyapuuze matokeo ya uchaguzi huu. Amesema anaamini matokeo ya uchaguzi huu si kura ya kukiunga mkono chama cha Socialist bali ni onyo dhidi ya utawala wa rais Sarkozy.

Shirika la kutafuta maoni la Opinionway linasema asilimia 27 ya wafaransa walipiga kura kuiadhibu serikali kwa utendaji wake huku asilimia 56 wakisema hilo halikuwa muhimu kwao.

Waziri mkuu wa Ufaransa, Francois Fillon, amesema serikali itaendelea mbele na ajenda ya mageuzi ya rais Sarkozy pasipo kuzingatia matokeo ya awamu ya pili ya uchaguzi hapo Jumapili ijayo. Fillion amewashutumu wapinzani kwa kuchochea wasiwasi katika ngazi ya kitaifa kujaribu kujikingia kifua katika ngazi ya mashinani. Kiongozi huyo amesisitiza kwamba la muhimu lililopo ni usimamizi wa miji, vijiji na mikoa.

Kulikuwa na maeneo yaliyosisimua katika uchaguzi wa jana ikiwa ni pamoja na mji wa Bordeaux, ambako waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa, Alain Juppe, alichaguliwa tena kuwa meya wa mji huo. Vilevile kati ya mawaziri 13 waliogombea umeya, sita walichaguliwa lakini wengine saba wanasubiri awamu ya pili ya uchaguzi Jumapili ijayo.

Uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali za mitaa nchini Ufaransa unachukua nafasi muhimu kwa kuwa wanasiasa wengi wa kitaifa hutafuta kuchaguliwa wakiwa na matumaini ya kujijengea umaarufu wa madaraka katika maeneo ya mashinani.