1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani waitisha maandamano nchini Kenya

Josephat Charo 13 Januari 2008

Kati mkuu wa zamani bwana Kofi Annan kuongoza juhudi za upatanisho

https://p.dw.com/p/CoB2
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila OdingaPicha: AP

Upinzani nchini Kenya umeapa kufanya tena maandamano makubwa kufuatia kushindwa kwa juhudi za kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anaziunga mkono juhudi za katibu mkuu wa umoja huo aliyestaafu, bwana Kofi Annan, kujaribu kuutanzua mgogoro wa kisiasa nchini Kenya uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi. Marekani na Uingereza nazo pia zimekukaribisha kuteuliwa kwa bwana Kofi Annan kuongoza juhudi za upatanisho.

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya Orange Democratic Movement, ODM, Salim Lone, amesema imedhirika wazi kwamba serikali haina haja ya kuutanzua mgogoro wla kisiasa nchini Kenya. Kwa hiyo maandamano ambayo yalikuwa yamesitishwa yataanza tena kote nchini. Tangazo hilo linafuatia kuteuliwa kwa Kofi Annan kuendeleza juhudi za upatanisho nchini humo.

Marie Okabe, msemaji wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema kiongozi huyo alizungumza kwa simu na bwana Kofi Annan na kumwambia anamuunga mkono kwa dhati katika kazi yake mpya ya kuzipatisha pande zinazohasimiana nchini Kenya.

Akijibu maswali kuhusu jukumu la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi nchini Kenya, msemaji wa katibu mkuu wa umoja huo, Michele Montas, amesema umoja huo haukuwa na waangalizi wake katika uchaguzi huo wala wakati wa kuhesabiwa kwa kura. Kwa hiyo umoja wa Mataifa hauwezi kujiingiza sana katika swala ambalo haukuhusika na hauna ukweli kamili.

Rais wa Ghana John Kufuor aliyendoka jana mjini Nairobi kurejea Accra, baada ya juhudi za Umoja wa Afrika kutaka kuutanzua mzozo wa kisiasa nchini Kenya kukwama, amesema rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, walikubaliana jana kushirikiana na jopo litakaloongozwa na bwana Kofi Annan kuumaliza mzozo ambao umesababisha vifo vya mamia ya watu.

´Jambo la kutia moyo ni kwamba pande zote mbili zimekubaliana kwamba machafuko yakomeshwe na zinapinga machafuko. Na pia zimekubaliana kuwepo na mazungumzo yatakayoongozwa na jopo la Waafrika mashuhuri.´

Akizungumzia kuhusu swala la demokrasia nchini Kenya rai John Kufuor amesema

´Kila mtu anazungumzia demokraisia. Demokrasia inataka hata kama hamjakubaliana, mkubaliane kwamba hamjakubaliana. Lakini sio kufyatuliana risasi, kuua na kuharibu mali.´

Katibu mkuu wa chama cha ODM, profesa Anyang Nyong´o anamlaumu rais Kibaki kwa kuzikwamisha juhudi za rais Kufuor kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini Kenya.

´Chama cha ODM hakina wasiwasi kuhusu wakati. Ni Kibaki ndiye anayeishiwa na muda. Chama cha ODM hakisababishi hali ya wasiwasi miongoni mwa Wakenya, ni Kibaki ndiye anayefanya hivyo. Kuna mtu mmoja katika ikulu ambaye hataki nchi hii isonge mbele kwa sababu anataka madaraka.´

Marekani pia imekukaribisha kuteuliwa kwa bwana Kofi Annan kuendeleza juhudi za upatanisho nchini Kenya. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani Tom Casey, amesema Marekani inapongeza juhudi za Umoja wa Afrika kusaidia kujaribu kutafuta suluhisho la tofauti za kisiasa kati ya vyama na watu binafsi nchini Kenya. Aidha bwana Casey amesema uteuzi wa bwana Annan ni sehemu ya juhudi za pamoja zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa kujaribu tena kutafuta suluhisho la kisiasa.

Mjumbe maalumu wa Marekani, Jendayi Frazer, ambaye bado yumo mjini Nairobi, anatarajiwa kurejea nyumbani hivi karibuni. Hata hivyo Tom Casey amesema kurejea kwake hakupaswi kuonekana kana kwamba Marekani haina nia ya kusaidia kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa nchini Kenya.

Kiongozi huyo amesema Marekani itaendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na makundi mengine kuhakikisha makubaliano yanafikiwa kati ya vyama vya kisiasa. Marekani imetoa dola milioni tano kusaidia Wakenya walioathirika na waliolazimika kuyahama makazi yao kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi. Fedha hizo zitatolewa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kimataifa kusadia katika maswala ya afya pamoja na chakula, maji, usafi na mahema.

Uingereza nayo pia inaunga mkono uteuzi wa bwana Kofi Annan kusaidia kuzipatanisha pande zinazozozana nchini Kenya. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, David Miliband, amesisitiza haja ya kuchunguza madai ya wizi wa kura na kuwatolea mwito viongozi wa Kenya washiriki kikamilifu katika mchakato wa mariadhiano bila masharti na wakubaliane vipi watakavyogawa madaraka serikalini.